Na Penina Malundo,Timesmajira
VIONGOZI wa Dini nchini wametakiwa kuwa mstari mbele wa kuendelea kusimama katika maandiko matakatifu ya kumlinda mtoto wa kike kuingia kwenye ndoa za utotoni kabla ya umri wake kufikia.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki,Mchugaji Monica Lugome wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani katika mjadala wa kitaifa kujadili umri sahihi wa kuoa au kuolewa, mjadala uliowahusisha wadau mbalimbali kutoka kwenye mikoa 10 nchini ulioandaliwa na Taasisi ya kimataifa ya Norwegian Church Aid ikiwa ni maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia iliyoanza Novemba 25 hadi Desemba 10,2024.
Amesema viongozi wa dini wanawajibu na nafasi ya kusimamia maandiko hayo na kwamba watoto wa kike na wakiume wanatakiwa kupatiwa haki zao sawa huku mambo mengine wataendelea nayo pindi wanapokua.
Amesema Kanisa linaweka msisitizo zaidi kwa watoto kupatiwa haki zao zote za msingi ikiwa elimu,afya bora na matibabu ili waweze kuja kutimiza ndoto zao.
”Tunajitahidi kulea mtoto katika njia sahihi,ila tunatamani katika masuala ya ndoa kuhakikisha hatuwaozeshi watoto wetu wakiwa na umri mdogo kujiendeleza kufika mahali ambapo umri wake utamruhusu kuingia katika ndoa,sisi kama kanisa hatuungi mkono ndoa za utotoni tunatamani mtoto akue mpaka atakapokuwa mkubwa aingie katika ndoa.
”Mkutano huu ni muhimu unaoelezea agenda za kumlinda mtoto wa kike kwaajili ya kuepukana ndoa za utotoni sisi kwa upande wa kanisa bado neno la Mugngu linatuagiza Kumlea mtoto katika njia ipasayo na yeye hataiacha hata akiwa mzee ,tunaposema kumlea mtoto njia ipasayo ni kuhakikisha mtoto anapata haki zake katika nyanja zote ikiwemo elimu.
Kwa Upande wake Mkuu wa Chuo cha Songea Catholic Institute of Technical EducationPadri Longino Rutangwelera amesema kanisa Katoliki haliungi mkono ndoa hizo, akieleza maana ya ndoa katika mustakabali wa dini.
Amesema katika dini ndoa ni maagano ya watu wawili waliokomaa kimwili na kiakili na si vinginevyo.”Ndoa ina wajibu wake, misingi na haki zake, inamtaka mtu awe na ukomavu wa kiakili na kiimani pia, unapomlazimisha msichana kuingia kwenye ndoa za utotoni unapingana na uhalisia,” alisema padri huyo ambaye pia ni mwezeshaji katika tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania.
“Kumuoza binti ambaye hajakomaa kiakili, kimwili na kifikra ni kupingana na matakwa na mapenzi ya Mungu na kupingana na uhalisia kwani unapomlazimisha mtoto kuingia katika ndoa anakosa elimu na kuingizwa kwenye makubaliano ambayo kwa akili na ukomavu wake hana uelewa wa kutosha, hivyo atapata watoto wakati uwezo wake wa kuwa mama au baba hautoshi, ni vema wakaachwa hadi wawe wakomavu, kimwili, kiakili na kihisia ili kupokea majukumu hayo kikamilifu,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema kuna umuhimu wa kutenda uadilifu kwa kuwapa nafasi sawa watoto wa kiume na wa kike, ikiwamo suala zima la kupata elimu kwa kadri ya uwezo wao.
“Hata hivyo, bado kuna changamoto kwa mtoto wa kike, ikiwamo ya kuozwa katika umri mdogo na kukosa haki yake ya kielimu…ninachokitamani ili kuondoa ukatili huu, kuwepo na sheria ambayo itamsaidia mtoto wa kike kutoingia kwenye ndoa za utotoni,” amesema.
Aidha Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative,Rebecca Gyumi amesema wamekutana katika mkutano huo na viongozi wa dini kutoka zaidi ya mikoa 10,kujadili namna ya mchango wao katika suala la umri wa chini wa kuolewa na kuoa kwa watoto wa kike na kiume.
Alisema pia wamepata fursa ya kuangalia kwa mapana yake uzoefu wa nchi mbalimbali katika masuala ya mabadiliko ya ndoa.”Msichana Initiave katika kazi tuliyokuwa tunafanya hasa katika haki za mtoto wa kike tunafikiri kuwashirikisha viongozi wa dini ni muhimu sana kwani wanaushawishi mkubwa na wanafikia kundi kubwa la watu na wanauwezo wa kuliangalia suala hili kwa kulibeba na kuleta mabadiliko,”amesema.
Rachel Boma kutoka Shirika la UN Woman Tanzania alisema nchi mbalimbali zimefanya mabadiliko ya kisheria na kuweka umri wa ndoa kuwa ni miaka 18.”Nchi kama Indonesia au Misri ambazo mfumo wao wa sheria ni kama kwetu, Serikali iliona mabadiliko katika sheria zao na wao umri wa kuolewa ni miaka 18, hivyo katika mijadala kama hii tuna vitu vingi vya kujifunza kutoka kwa wenzetu.”amesema
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais