September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa Dini Mkalama waaswa kutoa elimu ya uchunguzi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali amewataka viongozi wa dini wilayani hapa kutumia vyema nafasi zao kuelemisha wananchi kuhusu kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuhubiri maadili mema nchini.

Wito huo ameutoa Septemba 20,2024 wakati wa kikao na viongozi wa dini mbalimbali wilayani hapa kwa ajili ya kujadili masuala yanayohusu mmonyoko wa maadili, suala la uzalendo, amani pamoja na ushiriki wa viongozi hao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Ningependa kutumia nafasi hii kuwataka mkawajuze waumini kuhusu kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakofanyika tarehe 27.11.2024 kwa amani na upendo. Tujitokeze kwa wingi katika kampeni, tujiandikishe kwenye daftari la Orodha ya wapiga Kura kuanzia Oktoba 11-20, 2024 lakini pia siku ya uchaguzi tuchague viongizi wetu kwa amani”amesema Machali


Vile vile Moses Machali amewakumbusha viongozi hao wa dini kuhusu zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutumia nafasi zao kuwaeleza wananchi ifikapo Septemba 25,2024 wajitokeze kuboresha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu kwa mwaka 2025.

“Uboreshaji utafanyika kwa siku saba kuanzia Septemba 25- Oktoba 1,2024, hivyo tujikoze kwa wingi pia” amesema Machali

Akizungumzia kuhusu suala la maadili pamoja na amani nchini, Moses Machali amesema viongozi wa dini wanajukumu kubwa katika kuhubiri amani pamoja na kulinda maadili ya jamii za kitanzania.

“Twendeni tukahubiri amani na upendo kwa waumini wetu, nitashangaa siku nikisikia watu wa Mkalama wanagombana kwasababu ya dini, kila mmoja aheshimu imani ya mwenzake” Mhe. Machali”

Kwa upande wake Mchungaji Manase Msengi, kutoka kanisa la KKT Ushirika wa Nduguti, ambaye amezungumza kwa niaba ya viongozi hao, amemshukuru na kumpongeza Mkuu wa wilaya ya Mkalama kwa kukutana na viongozi wa dini kwa ajili ya kujadili masuala ya maadili, uzalendo na amani hasa katika kipindi hiki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka wananchi wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi