Na Martha Fatael, TimesMajira Online
Umoja wa viongozi wa dini Kanda ya Kaskazini umeweka maazimio saba ya kuendeleza amani ya nchi kwa kuhimiza maadili kwa jamii na kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuuunaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.
Akisoma maazimio hayo katika kongamano la amani, Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Kilimanjaro, Shehe Alhaj Awadhi Lema, amesema viongozi wa dini wamekubaliana kuwa na jukumu la kuhimiza watu wote waliojiandikisha kupiga kura kuhakiki majina yao na kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi.

Ambapo kongamano hilo limetilia mkazo haja ya makongamano ya amani kuwa endelevu na kufanyika mara kwa mara ili kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kudumisha utulivu, mshikamano na heshima kwa sheria za nchi.
Shehe Awadhi ameeleza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwaelimisha waumini wao juu ya haki na wajibu wa kila mmoja katika kulinda amani ya taifa, pia elimu hiyo iwe sehemu ya mafundisho ya kila siku misikitini, kanisani na kwenye mikusanyiko ya kijamii.
Katika azimio jingine, viongozi hao wamewahimiza Watanzania kuepuka aina yoyote ya uchochezi kupitia mitandao ya kijamii au vyombo vya habari.
Wamesema ni muhimu kutumia majukwaa hayo kwa kueneza ujumbe wa amani, mshikamano na heshima.
Aidha, viongozi hao wametoa wito kwa vyombo vya dola kuendelea kutumia hekima na busara katika kulinda amani ya taifa, hasa wakati wa uchaguzi, ambapo wamesema matumizi ya nguvu yanapaswa kuepukwa isipokuwa pale inapobidi kisheria ili kulinda utu na haki za raia.

Shehe Awadhi pia amesema viongozi wa dini wanaamini kuwa kuna haja ya kupanua wigo wa ushiriki wao katika vyombo vya kutunga sheria na kufanya maamuzi, ili kuongeza sauti ya maadili na maono ya kiroho katika uongozi wa taifa.
Azimio la saba limeeleza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kulinda amani hata anapodai haki zake,kwani hakuna haki itakayopatikana kwa njia ya vurugu na kila mtu anapaswa kuwa balozi wa amani ndani ya jamii.
Kwa upande wake,Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava akizungumza kwa baba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu,amesema viongozi wa dini wanapaswa kuendelea kuwa mstari wa mbele kuimarisha misingi ya maadili na mshikamano wa taifa.
Mnzava, amesema ni wajibu wa jamii, viongozi wa dini na serikali kuhubiri amani kwani ndiyo msingi wa maendeleo huku akisisitiza kuwa hali ya usalama ya mkoa ni shwari wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo kutimiza haki yao ya kupiga kura.
Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaban Mlewa, amesema kongamano hilo la amani lenye kaulimbiu,“Kupiga kura ni haki yetu, na amani ya taifa letu ni wajibu wetu”, linatoa ujumbe muhimu kwa kila Mtanzania kutambua nafasi yake katika kulinda amani.
Amesema kuwa uzalendo hauishii kwenye mapenzi ya nchi pekee, bali ni pamoja na kuchukua hatua za kulinda misingi ya haki, usawa, na heshima ya kila raia.Ambapo amani ni agizo la Mungu na tunu ya taifa ambayo lazima ilindwe kwa gharama yoyote
“Uzalendo ndio unaochochea amani, na amani huleta maendeleo,msingi wake ni ulinzi wa watu, nafsi na mali bila dhuluma,” amesema Shehe Mlewa.
Mwakilishi wa Askofu Dk. Fredrick Shoo, Mchungaji Daniel Swai, anasema jamii yoyote inayotanguliza amani hufanikisha maendeleo kwa haraka.
Amesema haki hupatikana kirahisi zaidi katika mazingira ya utulivu kuliko kwenye migogoro au vurugu.



More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi