Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga
VIONGOZI waUshirika mkoani Rukwa wanapata mafunzo ili vyama vya msingi vya ushirika viweze kusimamia kwa ufanisi matumizi ya matrekta kama ilivyoainishwa katika mpango wa kuinua sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDPII).
Mafunzo hayo yanatolewa kabla ya Kampuni ya Agricom Africa Company Limited kutoa matrekta kwa vyama vya msingi vya ushirika ili kuinua uzalishaji wa mahindi katika kila wilaya ya mkoa wa Mpanda.
Kwa mujibu wa programu hii chama cha msingi chenye wananchama wanaozidi 72 ambacho kitakuwa na fedha ya awali ya kulipia matrekta kitapewa matrekta ili kuinua uzalishaji wa mazao na kuinua kipato cha wakulima kama ASDP II inavyotaka.
Akizindua mafunzo hayo hapa jana Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Ocram Chengula, ameisifu kampuni ya Agricom Africa kwamba inatekeleza kwa vitendo programu ya ASDP II.
“ASDP II imejielekeza katika kuhakikisha matumizi ya zana bora za kilimo zinawafikia wakulima nchini ili kuongeza tija ya uzalishaji mazao nchini. Kampuni hii ASDP II kwa vitendo,” alisema Chengula
Alisema asilimia kubwa ya wakulima wa Rukwa wanatumia jembe, wanyama kazi na wachache wanatumia matrekta na kuongeza kwamba mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuanza kutumia zana za kisasa katika na kuinua kilimo biashara, na kuongeza kwamba uzinduzi wa programu hiyo utaongeza hamasa ya uzalishaji wa mazao hususani mahindi na kuufanya mkoa kujitosheleza kwa chakula na kuuza ili kuinua kipato cha wakulima.
Mkoa wa Rukwa una hekta 574,291 nzuri za kilimo ambazo kwa kiasi kikubwa zinamilikiwa na wanachama wa vyama vya msingi vya ushiriaka.
Kwa kawaida hekta 303,393 kila mwaka hupandwa mazao ya nafaka na mboga. Kati ya hizo, hekta 1,049 (au asilimia 0.3) hupandwa mazao wakati wa vuli na hekta 302,345 (aslimia 99.7) hupandwa mazao wakati wa masika.
Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Agricom Africa, Remmy Nindi, amesema kampuni yake inaelewa mkoa wa Rukwa una fursa kubwa za uzalishaji wa mazao ya mahindi.
“Rukwa ina nafasi kubwa ya uzalishaji kwa wingi zao la mahindi kutokana na ardhi yake kuwa na rutuba, hivyo kwa kuwapatia elimu ya matumizi ya zana za kisasa za kilimo kutaongeza uzalishaji mara tatu ya walivyokuwa wakizalisha awali,” alisema Nindi.
Alisema kampuni yao ina matawi Morogoro,Mbeya,Dodoma na Kahama. Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, Benjamin Mangwala, alisema ofisi yake itahakikisha matumizi sahihi ya zana za kilimo zitakazo milikiwa na vyama vya msingi vya ushirika ili kuwaletea maendeleo wanachama wa vyama hivyo.
“Tutaandaa mwongozo wa namna bora ya kusimamia matumizi ya zana hizi katika vyama vya ushirika ili wanachama wake waweze kunufaika na pia iwe sehemu ya kuwaongezea kipato katika vyama kwa kutumia zana hizo katika shughuli mbalimbali,” alisema Mangwala
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati