January 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi TANAPA wapigwa msasa usimamizi wa vihatarishi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

VIONGOZI wa Idara mbalimbali ndani ya Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), wameanza mafunzo maalum ya siku tatu kuanzia leo hadi Januari 31, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara.

Mafunzo hayo yanahusu Uhamasishaji wa Usimamizi wa Vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa TANAPA (Risk Management).

Akifungua mafunzo hayo leo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Massana Mwishawa amewataka viongozi hao kutambua jukumu kubwa la kusimamia na kupunguza vihatarishi ili kutekeleza majukumu ya Shirika kwa ufanisi mkubwa

“Lengo la mafunzo haya ni kuwapatia zana za vitendo, maarifa, na mikakati ambayo itatumika kuboresha usimamizi wa vihatarishi katika taasisi nzima.

“TANAPA tunatekeleza muongozo wa usimamizi wa viatarishi (Enterprise Risk Management Framework and Policy 2024/2025 – 2028/2029).

“Mafuzo ya leo yameandaliwa ili kuongeza uelewa wetu kuhusu umuhimu wa usimamizi wa vihatarishi, sio tu kama kazi, bali kama chombo cha kimkakati kinacholingana na malengo yetu na kuboresha michakato yetu ya maamuzi,” amesema Kamishna Mwishawa.

Aidha, Kamishna Mwishawa ameongeza kuwa, vihatarishi ni jambo lisiloweza kuepukika. Hivyo, ni muhimu kila mmoja wetu hasa wale walioko katika nafasi za uongozi kuwa na uelewa thabiti wa jinsi ya kushughulikia changamoto hizi kwa ufanisi.

Pia, amesisitiza maandalizi ya bajeti za mwaka wa fedha 2025/2026 inapaswa kuzingatia vihatarishi, pamoja na hatua na mikakati ya kupunguza vihatarishi yaani “Risk based budgeting”

Mafunzo haya ya siku tatu ya usimamizi wa vihatarishi yanaendeshwa na Dkt.Bernard Mnzava kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).