April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi dini wahimizwa kuelimisha jamii madhara ya rushwa katika uchaguzi

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt.Batilida Buriani, amewahimiza viongozi wa dini kuibeba agenda ya uchaguzi mkuu mwaka huu kwenye majukwaa yao na kuhakikisha viongozi wanaotaka kuingia madarakani kwa njia ya rushwa hawapenyi.

Balozi Dkt.Batilida ametoa kauli hiyo wakati akifungua semina kwa viongozi wa dini iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)Mkoa Tanga, ambapo amewahimiza viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kuielimisha jamii umuhimu wa kupambana na rushwa na kushiriki katika uchaguzi kwa lengo la kuwapata viongozi bora.

Pia kutumia nafasi zao katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba za ibada kuendelea kukemea vitendo vya rushwa hususani kipindi hiki taifa linapojiandaa kuelekea uchaguzi mkuu wa kupata Rais , Wabunge na Madiwani.

“Kama mnavyofahamu maadui wa kubwa wa maendeleo katika nchi yeyote ni rushwa ambayo ni adui wa haki mwaka huu ni wa uchaguzi,niwaombe muendelee kuliombea taifa amani Taifa letu,”.

Kwa upande wake Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwatah amesema taasisis hiyo imeamua kuwakutanisha viongozi hao kwa kutambua umuhimu wao kwa jamii.

Pia amesema kupitia uchaguzi wa Serikali za mitaa , vijiji na vitongoji uliofanyika Novembe 2024, walibaini baadhi ya vitendo vya rushwa ambavyo walivichukulia hatua.Hivyo kuelekea uchaguzi mkuu viongozi wa dini wana nafasi ya kushiriki katika kampeni ya mapambano dhidi ya rushwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Tanga,Sheikh Juma Ruuchu, amewahimiza viongozi wa dini kupelekea ujumbe huo kwa wananchi.

“Jambo hili bado linaleta shida katika nchi yetu,tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano na kupeleka ujumbe wa elimu hii kwa waumini na wananchi,”.