March 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi CHADEMA, Odinga wakutana, wajadili hali ya kisiasa nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamewasili jijini Nairobi, Kenya, mwishoni mwa wiki kwa mazungumzo na kiongozi mkongwe wa siasa za upinzani nchini humo, Raila Amolo Odinga.

Katika ujumbe huo uliojumuisha Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Bara, John Heche, na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, walikutana na Odinga ofisini kwake siku ya jumamosi kujadili hali ya kisiasa nchini Tanzania na harakati za mapambano ya kidemokrasia zinazoongozwa na chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CHADEMA kupitia akaunti yake rasmi ya mitandao ya kijamii ya X(zamani Twitter), viongozi hao walipata fursa ya kumweleza Odinga juu ya msimamo wa chama chao wa “No Reform, No Election”, ambao unalenga kutoshiriki uchaguzi wowote mpaka kuwe na marekebisho ya mfumo wa uchaguzi nchini Tanzania.

Aidha, walipata nafasi ya kupokea uzoefu na ushauri wa kisiasa kutoka kwa Odinga, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika harakati za demokrasia nchini Kenya kwa miongo kadhaa.

Kwa upande wake Raila Odinga ambaye pia aliweka chapisho katika mtandao wa X (zamani Twitter) akieleza mawazo yake kuhusu jukumu muhimu la kisiasa katika maendeleo ya Taifa, Odinga alisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kujenga kati ya makundi ya upinzani na serikali husika.

Katika mazungumzo hayo, Odinga alionyesha matumaini kuhusu uchaguzi ujao wa Tanzania, akisema, “Natarajia uchaguzi wa amani na uwazi katika uchaguzi ujao wa Tanzania.”

Odinga alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyama vya kisiasa ili kuhakikisha mchakato wa kidemokrasia una nguvu na kuomba wageni kuhusika kwa kujenga mazungumzo na serikali ya Tanzania kwa ajili ya manufaa ya taifa.

Aidha chapisho hilo lililogusababisha wachangiaji mbalimbali kutoa michango mseto liliambatanisha pia wafuasi na wachambuzi wa kisiasa. Wengi walimpongeza Odinga kwa kuhimiza mazungumzo na umoja kati ya viongozi wa upinzani, wakiona juhudi zake kama mwanga wa matumaini kwa thamani za kidemokrasia katika Afrika Mashariki.

Mmoja wa wafuasi alisema, “Huu ndiyo uongozi tunahitaji Afrika! Mazungumzo wazi yanaweza kujenga daraja na kuleta usalama kwa michakato yetu ya kidemokrasia.”

Chapisho la CHADEMA lilipokelewa kwa hisia tofauti na wachangiaji katika mitandao ya kijamii ambao waliweka wazi michango yao.

Baadhi ya michango hiyo ni pamoja na mchango wa Mama Ndege ambaye aliandika: “Raila ni mtu sahihi wa kutoa ushauri kwa wapinzani wa Tanzania. Amepambana sana Kenya, ana uzoefu mkubwa.”

Mchangiaji mwingine MzalendoTz: alielezaz kuwa “Sasa hivi ni wakati wa siasa za ndani! Badala ya kwenda Kenya, bora wakutane na Watanzania wanaoumia na hali ya sasa!”

Kwa upande wake Juma Mwinyi kupitia mchango wake kwenye chapisho hilo alisema “CHADEMA wanazidi kuthibitisha kuwa wao ni chama cha watu wanaojua siasa za kimataifa. Hii ni hatua muhimu kwa demokrasia ya Tanzania!”

MakaveliJnr: “Tundu Lissu na wenzake wanapaswa kujifunza kuwa siasa ni zaidi ya maandamano na migomo. Wanapaswa pia kuja na suluhisho la kisiasa lenye tija.”

Hatua hii ya viongozi wa CHADEMA inaonyesha jinsi ambavyo chama hicho kinaendelea kushirikiana na wanasiasa wa kikanda ili kupata mbinu mpya za kisiasa na kuimarisha harakati za demokrasia nchini Tanzania.