November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi CCM watakiwa kusimamia rasilimali za chama

Na Patrick Mabula , Kahama.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa , Fadhil Maganya amewaagiza viongozi kusimamia raslimali za jumuiya ziweze kuwa na tija.

Maganya ametoa agizo hilo leo wilayani Kahama kwenye ziara yake ya siku mbili ya kikazi ya kukangua mali na raslimali na uwekezaji wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Kahama ziweze kuleta tija.

Maganya amesema amebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika kusimamia mali na raslimali za Jumuiya hiyo na kuwaagiza viongozi kuhakikisha wanasimamia mali zote na miradi iweze kuwa na tija.

Amesema kuwa Jumuiya ya Wazazi ya CCM ina mali na raslimali na miradi mingi ambazo zikisimamiwa ipasavyo italeta tija na faida nyingi ambazo zitasaidia na kuweza kujiendesha.

“ Ndugu zangu viongozi kwa sasa nimeona kuna haja ya kutembea nchi nzima kuona mali na raslimali zote na miradi ya Jumuiya pale zilipo na zinaendeshwaje katika kujiletea mapato na kuisaidia Jumuiya,”Amesema Maganya alipokuwa akiongea na Viongozi

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo wa wilaya ya Kahama , Charles Nyanda amekiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika raslimali na miradi ya uzalishaji wa mali na maono na maagizo yake watayafanyia kazi.