January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi CCM ngazi ya matawi watakiwa kuhakikisha kadi zinawafikia wanachama

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya matawi na mashina Kata ya Kahama wametakiwa kuhakikisha kadi za kieletroniki zinazotolewa na chama hicho kuwafikia wanachama husika.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kahama Matayo Nicholaus wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya kata hiyo chenye lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za chama kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2023.

Ambapo amesema kuwa kupitia ziara za kamati ya siasa wamegundua kuwa na udororaji wa uhai wa jumuiya za chama hicho unaochangiwa na uhaba wa kadi za wanachama na uzembe wa baadhi ya viongozi kutowapa wanachama wapya na wa zamani kadi zao.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi niwaombe sana tuimarishe uhai wa chama chetu hizi kadi za kieletroniki zikawafikie wanachama wenyewe haraka iwezekanavyo,”amesema Matayo.

Pia amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa wananchi pamoja na kuitisha vikao ili wajue kinachotekelezwa na serikali yao.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Kata ya Kahama Petro Masune ameeleza kuwa kata hiyo ina jumla ya matawi manne yanayounda mitaa tisa na jumla ya wanachama wasiopungua 4018 kati yao wanaume 1654 na wanawake 2364 huku 540 pekee wakisajiliwa katika mfumo wa kieletroniki.

Huku akieleza kuwa chama hicho kina mkakati wa kuhakikisha kinashinda uchaguzi ujao, kujenga ofisi za matawi na kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Naye Diwani wa Kata ya Kahama Samwel Buchenja amesema kuwa kata hiyo imetekeleza miradi yenye thamani ya zaidi ya milioni 946 kupitia mapato ya ndani na Serikali Kuu ikiwemo ujenzi ya matundu ya vyoo shule ya msingi Lukobe, ujenzi wa madarasa shule ya sekondari Lukobe, ujenzi wa jengo la maabara zahanati ya Kahama, utengenezaji wa viti na meza shule mpya ya sekondari Masanza.

Muasisi wa CCM Kata ya Kahama ambapo Charles Mayala,amewapongeza viongozi wa chama wa kata hiyo kwa mtindo wao wa uongozi unaoshirikisha watu wote sanjari na kuwataka kuendelea na utaratibu waliouweka wa kuhakikisha wanatembelea kila mtaa kusikiliza na kutatua kero za wanachama