January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi 36 wa Uamsho huru DPP awafutia kesi ya ugaidi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP) amewafutia mashtaka viongozi wote 36 wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi na mchakato unaoendelea kwa sasa ni kutoka gerezani

Baada ya uamuzi huo, viongozi wawili kati ya 36 ambao ni Sheikh Farid Hadi Ahmed na Mselem Ali Mselem wameachiwa.

Mtandao mmoja wa kijamii jana ulimnukuu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu, akithibitisha kuwafutia mashtaka viongozi wote wa jumuiya hiyo na kwamba kilichobaki ni taratibu za kutoka gerezani.

Sheikh Farid Hadi Ahmed na Mselem Ali Mselem na wenzao 34 walikuwa mahabusu tangu mwaka 2014 wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha sheria ya kuzuia ugaidi ya 2002 Januari 2013 na Juni 2014.

Habari zaidi zilieleza kuwa masheikh hao wawili waliachiwa huru juzi baada ya DPP kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Awali, taarifa za kuachiwa kwa viongozi hao zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia jana jioni zikieleza kuwa viongozi hao wawili ndio wameachiwa huru na mmoja wa mawakili wao.

DPP alinukuliwa na mtandao huo wa kijamii akisema viongozi hao wameachiwa huru. Alisema amewafutia wote mashtaka yaliyokuwa yanawakabili na kwamba suala la kutoka gerezani kama wameshatoka wote au wangapi hilo ni suala la taratibu za Magereza, lakini amewafutia mashtaka wote.

Kwa mara ya kwanza walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na badaye kesi yao kuhamishiwa Mahakama Kuu.

Aprili 23, 2021 Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka 14 baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wao, Daimu Halfani, Juma Nassoro, Jeremiah Mtobesya na Abubakar Salum kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo kwa kuwa makosa wanayotuhumiwa yanadaiwa kutendeka Zanzibar.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake huo uliotolewa na Jaji Mustapha Ismail baada ya kusikiliza hoja za pande zote, hoja za pingamizi la utetezi na majibu ya upande wa mashtaka ulioongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga akisaidiwa na wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Paul Kadushi, ilikubaliana na hoja za utetezi.

Jaji Ismail alisema pamoja na mambo mengine kwa makosa ambayo yanadaiwa kutendeka Zanzibar, jukwaa sahihi la kuwashtaki washtakiwa ni katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Jaji Ismail aliuamuru upande wa mashaka kufafanua marekebisho katika hati ya mashtaka kwa kuyaondoa mashtaka hayo na kubakiza yale ambayo yamedaiwa kutendeka katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tanzania Bara ambayo ndio mahakama hiyo ina uwezo wa kuyasikiliza.

Akizungumza wakati akihojiwa baada ya kuachiwa, mmoja wa mashekh hao alisema kwa busara za Rais wa Zanzibar wetu wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan zimesaidia sana kumaliza mtanziko huo.

“Viongozi wetu wameafanya msaada mkubwa sana kuhakikisha waweza kuondoka kwa hali hiyo ya mtanziko. Tunamuomba mwenyezi Mungu amuongezee busara Rais Samia,” alisema.

Akizungumzia uamuzi huo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema amepokea ujumbe wa Sheikh Farid, wako nyumbani Zanzibar.