November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vikwazo nishati safi kuchunguzwa

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

SERIKALI imetangaza kuandaa kongamano la nishati safi ya kupikia (Clean Cooking Conference) ili kuchunguza vikwazo vinayodumaza matumizi ya nishati za kisasa za kupikia.

Kongamano hilo linalenga kupendekeza mikakati ya kufanikisha upatikanaji wa nishati safi, za bei nafuu na endelevu nchini Tanzania.

Kongamano hilo ambalo Rais Samia atakuwa mgeni rasmi linalenga kupendekeza mikakati ya kufanikisha upatikanaji wa nishati safi, za bei nafuu na endelevu nchini Tanzania.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nishati, January Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari jana. Alisema kongamano hilo litafanyika Novemba 1 na 2 mwaka huu na kuwakutanisha watunga sera, wadau wa maendeleo, wajasiriamali, wawekezaji, wafadhili, wanataaluma na wananchi kwa ujumla.

Alisema asilimia 72 ya nishati yote inayozalishwa nchini Tanzania inatumika majumbani na tungamotaka inachangia karibu asilimia 90 ya nishati yote inayotumika kwenye kaya.

Alifafanua kuwa asilimia 63.5 ya kaya zote nchini hutumia kuni kupikia na asilimia 26.2 hutumia mkaa. Sehemu iliyobaki inajumuisha asilimia 5.1 ya kaya zinazotumia gesi za mitungi, asilimia 3 umeme, na asilimia 2.2 ikiwa ni nishati nyingine.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, January Makamba, Waziri wa Nishati alisema, “Kupika ni moja ya tukio pekee linalounganisha watu wa hali zote: wa juu, kati na chini, ila Watanzania wengi hatujui na wala hatuhoji aina ya nishati inayotumika katika kupika vyakula tunavyokula kila siku”.

Matumizi ya nishati ya tungamotaka kupikia yanahusishwa na madhara mbalimbali ya afya ikiwemo magonjwa ya mfumo wa upumuaji, uharibifu wa mimba na vifo vya watoto wachanga.

Alisema takriban watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka nchini Tanzania kutokana na magonjwa yanayotokana na nishati chafu za kupikia zinazotumiwa majumbani ikiwemo kuni na mkaa. Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa janga hili.

Katika mkutano huo huo, Dkt. Pauline Chale, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mtaalam wa magonjwa ya kupumua alisema, “Tunatibu wagonjwa walioathirika na matumizi ya kuni na mkaa.

Matibabu haya ni ya muda mrefu na yanatumia rasilimali nyingi ambayo ingeweza kutumika kutibu wagonjwa wengine.”

Alisema mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi siyo tu ni wajibu wa kitaifa kuendana na lengo la 7 la malengo endelevu ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa (SDG7), lakini pia Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 unaelekeza serikali kuwezesha upatikanaji wa nishati salama, ya bei nafuu na ya kisasa kwa kupikia. Kwa hiyo, serikali imetenga shilingi milioni 500 kuwezesha upokeaji haraka wa nishati safi na ya uhakika.

Kwa kutambua haja ya hatua kuchukuliwa, wizara imeamua kuandaa kongamano litakalochochea mjadala kitaifa. Katika kongamano hilo, wataalamu kutoka sekta za umma na binafsi watajadili masuala mbalimbali kuhusu hali ya kupika nchini Tanzania; kubadilishana uzoefu kuhusu nishati safi za kupikia; kutathmini sera, sheria, udhibiti, uwezeshaji wa kifedha na teknolojia ili kukabiliana na changamoto. Kongamano linategemewa kujenga ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau.

Mabadiliko hayo yatakuwa na matokea chanya maishani mwa wananchi kiafya, kiuchumi na kimaslahi. Mabadiliko haya pia yatajenga fursa mpya za biashara na ajira na kuwezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo. Siku ya ufunguzi wa kongamano itahudhuriwa na Samia Suluhu Hassan.