December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vikundi kinamama wanaonyonyesha watoa msaada Muhimbili

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Hospitali ya Taifa Muhimbili imepokea msaada wa vitu mbalimbali wenye thamani ya TZS. 10Mil. kutoka vikundi vya kinamama wanaonyonyesha (Small Steps: Big Impact na Nutriplus Breastfeeding Support Group) ili kusaidia watoto waliozaliwa kabla ya wakati.

Vikundi hivyo vimetoa msaada wa chakula tiba kinachosaidia kuchochea maziwa ya mama kopo 400, vifaa maalum vya kuhifadhia maziwa, pampers na kulipia gharama za matibabu kwa kinamama tisa waliojifungua kabla ya wakati.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Meneja wa Jengo la Wazazi, Bi. Silviana Swallo amevipongeza vikundi hivyo na kusema kuwa msaada huo utawasaidia watoto ambao wamezaliwa kabla ya wakati kama ilivyokusudiwa.

Bi. Swallo amesema pamoja na kwamba Hospitali inajitahidi kutoa misamaha kwa watu wasio na uwezo bado uhitaji ni mkubwa kwakuwa hata wale wanaopunguziwa gharama za matibabu bado wanashindwa na kuiomba jamii kuendelea kutoa msaada kwa makundi ya namna hiyo.

“Ukimsaidia mama ambaye hana uwezo, tambua kuwa umemsaidia mama huyo kwenda kupata nafasi ya kukaa na mtoto wake nyumbani na pia unafungua milango ya baraka kutoka mama huyo ambaye hawezi kumudu kuchangia gharama za matibabu”, amesema Bi. Swallo.

Mwanzilishi wa Kikundi cha Small Step: Big Impact Bi. Yusta Kasenge amesema kuwa lengo la kuanzisha kikundi hicho ni kutoa hamasa kwa kinamama wanaonyonyesha kwakuwa maziwa ya mama yana faida nyingi kiafya kwa watoto wachanga.

“Tunatambua kuwa maziwa ya mama yana umuhimu mkubwa, hivyo leo tumekuja kutoa msaada huu kwa kinamama waliojifungua kabla ya wakati ili nao wapate mwamko wakunyonyesha watoto wao” amesisitiza Bi.Kasenge.

Ameongeza kuwa vikundi hivyo vitaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanapata fursa ya kunyonya maziwa ya mama kama inavyotakiwa kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi 6 ya mwanzo.