Na Judith Ferdinand,TimesMajira online,Mwanza
JUMLA ya wakazi 10,971 wa vijiji vya Nyasenga, Nyampande, Kawekamo na Busulwangiri wilayani Sengerema mkoani Mwanza watanufaika na mradi wa maji Nyampande uliopo wilayani humo.
Ambao Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imekabidhi rasmi mradi huo wa maji wa Nyampande kwa Mamlaka ya Maji ya Sengerema (SEUWASA).
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Kijiji cha Nyampande, wilayani Sengerema mbele ya wananchi wa Nyampande wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Meneja Miradi wa MWAUWASA, Mhandisi Gogadi Mgwatu alisema,mradi huo ulikamilika tangu mwezi Machi, 2021 na ulikuwa kwenye majaribio kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa SEUWASA kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa Vijiji vya Nyasenga, Nyampande, Kawekamo na Busulwangiri.
Mhandisi Gogadi amesema,umetekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya HALEM Construction Company Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya Bilioni 1.9 ambayo ilitolewa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji.
Amesema,ujenzi wake ulisimamiwa na MWAUWASA kwa kushirikiana na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Sengerema ambapo utanufaisha jumla ya wakazi 10,971 wa vijiji hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole,amewataka wananchi hao kutunza na kulinda miundombinu ya mradi huo wa maji kwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
“Wananchi muwe walinzi wa mradi na kuepusha uharibifu wa miundombinu na kuepuka maunganisho yaliyo nje ya utaratibu,kujiungia maji kinyemela na maji yatumike kama malighafi ya kujiongezea kipato na fursa ya kiuchumi,” amesema Kipole.
Pia ameendelea kwa kuwahimiza wananchi watambue wajibu wao wa kulipia ankara za maji ili kuiwezesha SEUWASA kwenye uendeshaji wake sanjari na kutanua wigo wa utoaji huduma.
Pamoja na kuchangamkia mradi kwa kuomba kuunganishwa huduma kwenye kaya zao ili kuepusha usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata maji.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi