Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania bara vitafikiwa na huduma ya umeme.
Ameeleza hayo bungeni, jijini Dodoma tarehe 6 Septemba, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Masasi, Geofrey Mwambe ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye Vijiji vya Namikunda, Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na Kata ya Temeke.
Akijibu swali hilo, Kapinga amesema kuwa katika Jimbo la Masasi, Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo havikuwa na umeme ambapo hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2023, vijiji 11 vimeshawashwa umeme na vijiji 6 vitakamilika kabla ya mkataba wa Mkandarasi kuisha tarehe 31 Desemba, 2023.
Ameongeza kuwa, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na Chakama vimekwishawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa umeme.
Amesema kuwa, kwa sasa, zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya Temeke (Mkarango) bado linaendelea na nguzo tayari zimekwisha simamishwa katika kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato