📌 Kapinga asema TANESCO na REA zimejidhatiti kufikisha umeme maeneo ya kijamii
📌 Vitongoji havijasahaulika; 122 kati ya 421 vina umeme
📌 Upelekaji umeme viwandani, migodini na maeneo ya kilimo unaendelea
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga Julai 22, 2024 amewasha umeme shule ya sekondari Nyasa iliyopo kijiji cha Chimate Kata ya Chiwanda wilayani Nyasa mkoani Ruvuma na kueleza kuwa vijiji vyote wilayani humo vimepelekewa huduma ya nishati hiyo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chimate Kapinga amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zimejidhatiti kuhakikisha kuwa huduma ya umeme haiishii nyumbani bali inafika kwenye maeneo yote ya huduma za kijamii.
Ameongeza kuwa, kazi ya usambazaji umeme vijijini ilianza kwa kupeleka nishati hiyo ngazi ya vijiji na hivi sasa kazi zinaendelea kwenye vitongoji.
“Maendeleo mnayoyaona yanafanyika hapa yanaendelea kufanyika nchi nzima kwani dhamira ya serikali ni kupeleka umeme kwenye maeneo yote nchini,” amesisitiza Kapinga
Pia amesema serikali imejipanga kutekeleza miradi ya upelekaji nishati ya umeme kwenye vitongoji kwani maendeleo ni hatua hivyo vitongoji vyote vitafikiwa na huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi ya Umeme Vijijini (REA) Mkoa wa Ruvuma, Robert Dulle amesema Wilaya ya Nyasa ina jumla ya vijiji 84 ambapo vyote vimepata umeme.
Mhandisi Dulle amesema kati ya vitongoji 421, vitingoji 122 vimepata huduma ya umeme na kazi inaendelea kupeleka umeme vitongoji vilivyobaki.
Aidha, amesema kwa sasa REA inatekeleza miradi mitatu katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyasa.
Ametaja miradi hiyo kuwa ni REA awamu ya tatu mzunguko wa pili, upelekeji wa umeme katika viwanda,migodi na maeneo ya kilimo na mradi wa ujazilizi mzunguko wa pili c.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa