Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali ya Tanzania na Austria zimefanya mazungumzo yatakayowezesha vijana wa nchi hizo mbili kunufaika na fursa mbalimbali zikiwemo za ajira, elimu, kilimo na ujuzi.
Mazungumzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu chini ya taasisi zake ikiwemo NSSF, PSSSF, OSHA na WCF na kuongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi na Waziri wa Kazi na Uchumi wa nchi hiyo, Profesa Martin Kocher.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Katambi amesema katika mazungumzo hayo wamejikita zaidi katika kuongeza ushirikiano wa kimataifa baina ya nchi hizo, kuimarisha sekta za elimu ya ufundi pamoja masuala ya hifadhi ya jamii.
“Tumejadiliana kwenye mambo ya msingi ikiwemo kuangalia namna gani nchi yetu tunaweza tukaingia kwenye mahusiano na kufungua fursa za ajira hususan kwa vijana wa Kitanzania kwenda kufanyakazi katika taifa hilo kwa wale wataalamu na wasio wataalamu,” amesema Mhe. Katambi.
Amesema wameangalia namna ambavyo wataweza kubadilishana ujuzi wa masuala mbalimbali hususan katika sekta ya kilimo, viwanda, biashara ili kuwaongezea Watanzania kuwa na sifa za kuajiriwa kwenye maeneo mbalimbali.
Mhe. Katambi amesema kupitia mashirikiano hayo wataangalia namna gani Austria ilivyofanikiwa kupitia sekta ya hifadhi ya jamii ili waweze kujifunza.
Amesema Tanzania pia ina mahusiano mazuri na nchi hiyo kwenye masuala ya elimu ya ufundi na amali, ambapo Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha katika Halmashauri mbalimbali pamoja na Mikoa kwa ajili ya kujenga vyuo vya VETA nchi nzima.
Mhe. Katambi amesema kupitia mashirikiano ya nchi hizo vijana Watanzania pia wanaweza kunufaika na fursa za kwenda kusoma na kujifunza katika nchi hiyo.
Amesema baadaye kama wataenda vizuri kupitia timu ya watalaamu na majadiliano yaliyopo watafikia hatua ya kusaini makubaliano ya awali baina ya nchi hizo mbili na kuonesha maeneo ambayo watashirikiana kwa maslahi mapana ya vijana wa Tanzania.
Mhe. Katambi amesema ujumbe huo pia umepata fursa ya kukutana na sekta nyingine za Serikali ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yanayozalishwa nchini.
Naye, Profesa Kochar ameishukuru Serikali ya Tanzania na kuahidi kuwa Austria itaendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali hususan kazi, sekta ya hifadhi ya jamii, elimu, kilimo, biashara, ajira na miundombinu.
Amesema wanaamini kuwa endapo watashirikiana na Tanzania wataweza kuwapatia vijana elimu ya ufundi ambayo itawasaidia kupata fani mbalimbali zitakazowasaidia kujenga maisha yao na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.
Profesa Kochar amesema Tanzania kuna fursa nyingi hivyo wataongeza utaalamu kwenye masuala ya teknolojia, kuongeza ushirikiano na kuongeza ujuzi wa masuala mbalimbali hususan kupitia sekta ya kilimo, viwanda na biashara.
More Stories
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia