December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana watakiwa kumuenzi Nyerere kujifunza historia

Dotto Mwaibale,TimesMajira Online. Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amewataka vijana kuanza kufikiri katika muktadha wa kuongozwa na tafakuri ya kina kujua na kuona sawa-sawa historia ya Taifa la Tanzania lilipotoka, lilipo na linapoelekea.

Amesema kama vijana watafikiri sawasawa ni lazima watakuwa na upeo mkubwa wa jicho la kuona sawasawa mnyororo mzima wa hatua kadhaa za kimaendeleo, zilizofikiwa hatua kwa hatua tangu uhuru.

Nchimbi ametoa nasaha hizo wakati akizungumza na vijana mbalimbali, kupitia ‘Kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa 2020, lililofanyika kwenye Chuo cha Uhasibu mkoani hapa.

Mkuu huyo wa Mkoa amewaambia vijana kuwa bila ya kumfahamu vizuri na kumtazama Mwalimu Julius Nyerere, kamwe hawawezi kuwa kiunganishi mahiri kwenye mnyororo wa kiuchumi kutoka kwenye uchumi wa kati kwa sasa, kuelekea uchumi wa juu wa kati.

“Vijana ndiyo watendaji na kumbukeni miradi yote hii mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa, inafanyika kwa fedha zetu za ndani na zaidi ni kwa manufaa yenu vijana…fikirini sawasawa ili muone sawasawa,” amesema.