November 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana waitwa JKT, onyo dhidi ya matapeli latolewa

Na Joyce Kasiki, Dodoma

JESHI  la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza nafasi za kujiunga na mafunzo ya kujitolea kwa mwaka 2026/2027 kwa vijana wote wenye sifa kutoka Tanzania Bara na Visiwani , huku  likiwakaribisha vijana wenye elimu na ujuzi katika fani mbalimbali  kujiunga na Jeshi hilo.

Tangazo hilo linatoa fursa kwa vijana kutumia taaluma zao kupata mafunzo ya kijeshi na kujijengea nidhamu, uzalendo na ujuzi wa maisha.

Akitoa tangazo hilo Makao Makuu ya JKT, Mkuu wa Tawi la Utawala, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema nafasi hizo zinawalenga vijana wenye sifa zinazohitajika, hususan wenye Shahada ya Sayansi ya Mitandao ya Kompyuta na Usalama wa Taarifa pamoja na walimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo.

Ametaja fani zinazohitajika kuwa ni uchomeleaji, ufundi magari, umeme wa magari, ufundi bomba, ufundi rangi, uashi, TEHAMA, ubunifu wa mavazi, ukarani, useremala, ushonaji pamoja na ufundi wa friji na viyoyozi. Vijana wenye utaalamu katika maeneo hayo wanahimizwa kutumia fursa hiyo kuwasilisha maombi yao.

Kwa mujibu wa JKT, maombi yanapaswa kuwasilishwa kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Usaili wa waombaji unatarajiwa kuanza Novemba 16, 2026, katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku vijana watakaofaulu wakitakiwa kuripoti kambini kuanzia Desemba 10 hadi 15, mwaka huu.

Katika tangazo hilo, JKT limetoa onyo kwa vijana na wazazi kujihadhari na matapeli wanaoweza kutumia fursa hiyo kuwaibia wananchi. Brigedia Jenerali Mabena amesisitiza kuwa nafasi za mafunzo ya kujitolea JKT hazina malipo na hakuna mtu anayeruhusiwa kudai fedha ili kumsaidia mwombaji kupata nafasi.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapokutana na watu wanaodai kuwa na uwezo wa kuwapatia nafasi hizo kwa malipo, ili hatua za kisheria zichukuliwe. Pia amefafanua kuwa mafunzo hayo si dhamana ya kupata ajira serikalini au katika taasisi nyingine baada ya kuhitimu.

JKT limesisitiza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea vijana nidhamu, uzalendo, uwajibikaji na ujuzi mbalimbali utakaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.

Hivyo, vijana wenye sifa wanahimizwa kufuata utaratibu rasmi wa maombi na kuepuka kutoa fedha kwa watu wanaojifanya kuwa na ushawishi ndani ya Jeshi hilo.