March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana wahimizwa kuchangamkia fursa za kidigitali

*Binagi aiomba Serikali kupunguza gharama za usajili ili kutoa fursa kwa vijana 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza

Vijana wamehimizwa kuchangamkia fursa za kidigitali ikiwemo kuanzisha vyombo vya habari mtandaoni kama njia ya kujiajiri, huku Serikali ikiombwa kuona namna ya kupunguza gharama za usajili pamoja na kuondoa baadhi ya kodi zinazowaongezea mzigo watengenezaji wa maudhui.

Ombi hilo limetolewa Januari 24, 2026 na Mkurugenzi wa BMG Media, George Binagi, wakati wa hafla fupi ya kupokea tuzo maalum kutoka YouTube baada ya BMG Media kufikisha wafuasi (subscribers) laki moja.

Binagi amesema licha ya Serikali kupunguza gharama za usajili wa vyombo vya habari mtandaoni kutoka  milioni moja hadi  laki tano, kiwango hicho bado ni kikubwa kwa vijana wengi, hususani wahitimu wa uandishi wa habari.

“Naomba kiwango hicho kishushwe hadi laki moja ili kuwezesha vijana wengi zaidi kujiajiri,”amesema Binagi.

Hata hivyo amesema,kuwa kuanzia mwaka 2026, watengenezaji wa maudhui mtandaoni wameanza kukatwa asilimia tano ya mapato yao na kuwasilishwa serikalini, huku wakiendelea kulipa kodi nyingine, hali aliyosema imewaongezea mzigo wa kulipa kodi mara mbili.

“Hatupingi kulipa kodi, lakini mfumo uliopo kwa sasa unatubebesha mzigo mkubwa, hivyo tunaomba Serikali kulifanyia kazi suala hili,” amesema Binagi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MISA TAN ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko, amesema mitandao ya kijamii kwa sasa imekuwa fursa muhimu kwa vijana katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, na kuwataka kuitumia kwa njia sahihi, yenye maadili na tija.

Soko ameahidi  kufikisha  hoja za malalamiko ya gharama za usajili na kodi  kwa mamlaka husika kupitia vikao vya wadau wa habari vinavyoendelea kufanyika kwa lengo la kuboresha sekta ya habari nchini.