March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana wahimizwa kuchagamkia fursa za uwekezaji

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

TAASISI ya Serikali inayosimamia na kuendeleza mifuko ya uwekezaji pamoja (UTT Aims) Saimon Migangala, amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji kama njia ya kujenga na kuendesha maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Migangala ametoa wito huo Jijini Dar es salaam katika ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa Taasisi hiyo ambapo amesema kukuza mtaji kunahitaji kuanza kuwekeza kidogo kidogo na hatimaye kupata matokeo .

Amesema mfuko wa Umoja umeendelea kufanya vizuri kifedha baada ya kufikia faida ya zaidi ya asilimia 12, huku mifuko mingine ya uwekezaji ikirekodi ongezeko la zaidi ya asilimia 13.

“Kwa mwaka mmoja uliopita, UTT Aims imepata ukuaji wa zaidi ya shilingi trilioni moja, ukuaji ambao haujawahi kushuhudiwa tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa mwaka huu umekuwa mzuri sana kwetu, hususan kwa upande wa idadi ya wawekezaji, ambapo tumeshuhudia ongezeko kubwa,” amesema Migangala.

Amebainisha kuwa wakati UTT Aims inaanza, ilikuwa na wawekezaji wapatao laki tatu, lakini kwa sasa imefikia zaidi ya wawekezaji laki tano. Aidha, kwa mwaka mmoja uliopita pekee, taasisi hiyo imepata wawekezaji wapya zaidi ya laki moja na elfu 50.

Migangala amewashukuru wawekezaji wote walioanza na wanaoendelea kutumia huduma za uwekezaji za UTT Aims, akibainisha kuwa imani yao imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya taasisi hiyo.

Pia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini Tanzania, pamoja na wadau wote wanaoshiriki katika kuboresha mazingira ya uwekezaji.Hata hivyo, amesema taasisi hiyo inatambua kuwa bado kuna Watanzania wengi hawajafikiwa na huduma za uwekezaji, ndiyo maana jitihada zinaendelea kufanyika ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, ikiwemo kuongeza ofisi katika mikoa mbalimbali nchini.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya UTT Amis Profesa Faustin Kamuzora, amesema taasisi hiyo ina jukumu kubwa katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji.

Aidha amesema kuwa uwekezaji katika masoko ya mitaji ni nyenzo muhimu ya kuinua kipato cha Mtanzania na kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo 2050.