January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana wahamasishwa kufanya mazoezi

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amezindua klabu ya mazoezi ya Apao Eco Apao Eco ‘Apao Eco Jogging Club’ ikiwa na lengo la kuboresha afya, kuhifadhi na kujenga mazingira safi na salama.

Akizungumza katika uzinduzi wa klabu hiyo uliofanyika katika viwanja vya Apao Village Kigamboni Dkt. Ndugulile amesema, vijana wengi kwa sasa hawafanyi mazoezi, wanakula hovyo na wanakunywa pombe ovyo bila kufanya mazoezi bila kujali kuwa wanahatarisha afya zao.

Amesema, ni vema watu wakajenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuweza kujenga afya za miili yao na anaamini kupitia Apao Eco Jogging vijana watahamasika kufanya mazoezi ili kulinda afya zao na kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo kwa sasa yameshamiri.

“Tunachangamoto kwa vijana hatufanyi mazoezi, ukiangalia takwimu zetu sasa hivi vijana wa kiume na wa kike wanavitambi na hii ni utapiamlo na inatokana na kutokufanya  mazoezi lakini pia suala la mazingira nalo ni jambo jema ni vema kuendelea kuhamasishana huku kuhakikisha Jumamosi za usafi watu wanafanya usafi kwani usafi mzuri ukifanyika jamii itapiga hatua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuzuia  Magonjwa,”amesema Dkt. Ngugulile.

Miongoni mwa vijana walioshiriki uzinduzi wa klabu ya mazoezi ya Apao Eco wakiwa wanafanya zoezi la kuokota taka ikiwa moja ya lengo la uzinduzi wa Klabu hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Jielimishe Kwanza, Henry Kazula amesema, uzinduzi wa  klabu hiyo ya Apao Eco ni wa kwanza kwa  mbio za polepole kuzinduliwa chini yao hapa Tanzania kwa usimamizi wa Kampuni ya Jielimishe Kwanza ikishirikiana na ‘Apao Village Cultural Centre and Tourism Enterprise’ iliyopo Mbutu-Kigamboni.

“Jielimishe Kwanza ni Kampuni ya kipekee inayobuni miradi, kutoa mafunzo ya kuhifadhi Mazingira na kuwajengea vijana uwezo kutumia changamoto za sekta ya Mazingira kutengeneza fursa za biashara na ajira, imeamua kuja na Eco Jogging kwa lengo la kuhimiza jamii kujenga afya na kuhifadhi Mazingira,”.

“Tunataraji kuwa na Eco Jogging Klabu nyingi hapa Dar es Salaam na Tanzania, pamoja na kushirikiana na klabu nyingine zilizopo kuleta hamasa kwa jamii kudhibiti taka ngumu katika mazingira yetu tunakaribisha wadau mbali mbali wa maendeleo kushirikiana nasi ili tujenge afya kwa pamoja na kulinda mazingira kupitia mbio pole pole kwa mara ya kwanza kutokea Tanzania,” amesema Kazula.