Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amewaasa vijana nchini kukataa kutumiwa na watu wasioitakia mema nchi kuvuruga amani na utulivu wa Watanzania kwa sababu yoyote ile.
Kihongosi ametoa rai hiyo alipokuwa akiongea na wananchi wilayani Urambo mkoani Tabora kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kitega Uchumi Mjini hapa.

Amesema kuwa Tanzania imejengwa katika misingi imara ya amani na utulivu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu kianzishwe 1977 kimeendelea kusimamia misingi hiyo kwa gharama huku kikihubiri amani, umoja na mshikamano.
“Katika hili, nawasihi vijana wenzangu msikubali kutumiwa na hawa vibaraka wasioitakia mema nchi yetu kuvuruga amani, umoja na mshikamano wa Watanzania, kataeni mambo ya ovyo, lindeni nchi yenu,”amesema Kihongosi.
Kihongozi amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na waasisi wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume, hivyo akawataka wanasiasa kuacha mihemuko yenye viasharia vya uvunjifu wa amani.
“Najua wana Urambo mnapenda maendeleo na mnajivunia mazuri yote yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na serikali yenu ya Chama Cha Mapinduzi, asiwepo mtu wa kuwavuruga, lindeni amani iliyopo,”amesema.
Amesisitiza kuwa CCM ni chama cha wananchi wote ndiyo maana kimeendelea kusimamia kwa dhati amani, upendo na mshikamano wa watanzania ili tunu hiyo ya amani iendelee kudumishwa nchini.
Ametaja baadhi ya mambo yaliyofanywa na serikali katika Wilaya hiyo kuwa ni kuboreshwa huduma za afya kwa kujengwa hospitali ya wilaya yenye miundombinu yote na kujengwa shule mpya za kisasa za msingi na sekondari.
Ujenzi wa vituo vya afya katika Kata mbalimbali, zahanati katika vijiji vyote,mradi mkubwa wa Maji wa Miji 28 unaogharimu shilingi bilioni 143, ujenzi wa bwawa la maji la Kalemela na kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji vyote.

Mbunge wa Jimbo la Urambo,Magreth Sitta amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kuwajali wana Urambo na kuwaletea mabilioni ya fedha kwa ajili ya kutekelezwa miradi ya maendeleo.


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama