September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana Makete wapewa elimu ya kujiajiri

Na David John, TimesMajira Online, Njombe

MKUU wa wilaya ya Makete mkoani Njombe, Veronica Kessy ametoa wito kwa vijana wanaomaliza Elimu ya Juu kuacha kufikiria ajira serikalini badala yake wajikite kwenye kujiajiri.

Akizungumzia hilo Veronica amesema, vijana wengi wanaotoka vyuoni wanafikiria kupata ajira serikalini lakini wanaweza kuanzisha vikundi kwa ajili ya kujiajiri ikiwemo kujikita kwenye ufugaji na kilimo.

Veronika ameyasema hayo katika maadhinisho ya siku ya chakula duniani ambayo yameambatana na maonyesho ya chakula lishe huku yakibeba kauli mbiu ikiwa “kesho njema hujengwa na lishe Bora endelevu.”

“Leo Tumetembelea kwa mkulima na mfugaji wa ng’ombe Joseph Kimwayeya aliyeko katika Kijiji hiki Cha Mji mwema kata ya mji Mwema ili kujionea namna anavyofuga Ng’ombe wa maziwa, tumepata elimu ya kutosha na tumeweza kumshauli mambo mbalimbali.

“Moja ya Mambo ambayo tumeweza kumshauli ni pamoja na kukamua maziwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kutumia mashine maalumu ambapo mashine inasaidia kutopoteza maziwa na pia tumemshauli kuwa mbolea inayotokana na kinyesi Cha Ng’ombe uzalisha nishati ya umeme.(BIOGAS),” amesema Veronica.

Veronica amesema, pia wamemshauli mfugaji huyo kuzalisha majani mbadala ambayo yatahifadhiwa na kutumika wakati wa kiangazi lakini pia kutumia ujuzi aliopata kuifundisha jamii iliyomzunguka.

Akizungumzia kuhusu vijana Veronica amesema, kwenye halmashauri kuna fursa ya fedha asilimia kumi ambazo zimetengwa na serikali kwa ajili ya makundi ya vijana, akina mama pamoja na wenye mahitaji maalum, hivyo watumie fursa hiyo kuweza kupata fedha na kukaa katika vikundi ili kufanya kilimo na ufugaji badala ya kufikiria kuajiliwa na Serikali na taasisi zingine.

Kwa upande wake mfugaji Joseph Kimwayeya, ameshukuru kwa kuona serikali wamekuja kumtembelea na kuona kile anachokifanya .”Naishukuru serikali kupitia Afisa Mifugo na ugani wamekuwa wakinipa ushauli wa kitalamu kuhusu ufugaji na kilimo “amesema Kumwayeya.

Ameongeza kuwa atazingatia maelekezo ya kitaalamu ambayo ameshauliwa na hasa kupata mashine za kukamua maziwa lakini kuzalisha majani kwa ajili cha malisho ya Ng’ombe kwa msimu wa kiangazi unapofika.

Naye katibu tawala wa mkoa wa Njombe Katarina Revocat, amewataka wananchi mkoani humo kuiga mfano wa mkulima na mfugaji Kimwayeya kwani mfugaji aliaza kufuga kutoka kwenye ndama wa miezi sita hadi leo kufikia Ng’ombe 15 wa maziwa .

%%%%%%%%%%%%%%%