March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana 168,657 wanufaika na programu ya Uanagenzi

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ,Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amefungua rasmi mafunzo ya uanagenzi yanayotekelezwa kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, ambayo mpaka sasa imewanufaisha vijana wapatao 168,657 huku akisitiza kuwa hatua hiyo ni mkakati mahsusi wa kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi na weledi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza leo Machi 3,2026 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo katika Chuo cha Ufundi cha Donbosco jijini Dodoma, Waziri Sangu amesema kuwa Taifa linahitaji nguvu kazi yenye ujuzi, inayotumia teknolojia na inayoweza kuhimili mabadiliko ya soko la ajira pamoja na kuchochea ubunifu na ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa.

Amesema mafunzo hayo hayalengi kuwajengea vijana maarifa ya darasani pekee, bali kuwaandaa kuingia katika ushindani wa ajira ndani na nje ya nchi.

“Tunataka vijana wa Kitanzania wanapokwenda kufanya kazi nje ya nchi wawe na uwezo unaolingana na vijana wengine duniani. Ndiyo maana tumeanzisha programu hii kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa, hususan wenye ujuzi wa chini, wanaongezewa stadi za kisasa,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa programu hiyo imejumuisha fani mbalimbali ili kuhakikisha sekta zote zinapata wataalamu wa kutosha watakaoshiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi.

“Lengo kuu ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2050, baada ya miaka 25 ya utekelezaji wa dira ya maendeleo, Tanzania inakuwa na wataalamu wenye ujuzi unaoakisi viwango vinavyohitajika kuendesha uchumi wa viwanda.”amesisitiza Naibu Waziri huyo

Aidha, amewataka wakuu wa vyuo na taasisi za mafunzo kuhakikisha wanatoa mafunzo yanayoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira ili wahitimu waweze kuajirika au kujiajiri.

Amehimiza vyuo kuchangamkia fursa hiyo na kupongeza taasisi zilizojitokeza, huku akieleza kuwa mwitikio bado ni hafifu.

Pia aliitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kushiriki kikamilifu katika utoaji wa mafunzo hayo ya uanagenzi ili kuongeza wigo wa wanufaika.

Amewaasa vijana kuitumia fursa hiyo kikamilifu katika kujipatia ujuzi utakaowakwamua kiuchumi pindi watakapohitimu mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus, amesema Ofisi hiyo inaendelea kutekeleza mafunzo ya uanagenzi kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kama hatua ya makusudi ya serikali ya kukabiliana na changamoto ya kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa nguvu kazi ya Taifa ambayo ni vijana.

Ameeleza kuwa programu hiyo ilianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa lengo la kukuza ujuzi wa nguvu kazi iliyopo katika soko la ajira ili kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.

Zuhura amesema hadi kufikia Februari 2026, jumla ya wanufaika 168,657 wamenufaika na programu hiyo, hatua inayoonesha dhamira ya serikali ya kuimarisha ushindani wa vijana katika soko la ajira na kukuza uchumi wa Taifa kupitia rasilimali watu yenye ujuzi.