November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana 150 kunufaika na mradi wa Agri Connect,Nyanda za Juu Kusini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira, Online,Mbeya

VIJANA 150 wabunifu kutoka mikoa ya Mbeya ,Iringa ,Katavi ,Songwe na Njombe wanatarajia kunufaika na mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani katika kilimo cha bustani za mbogamboga na matunda ambao ubunifu wao utashindanishwa na kuleta tija kwa taifa hususani kudhibiti upotevu wa mazao kuanzia shambani.

Akizungumza na Timesmajira Julai 28,2023 Mratibu wa Mradi wa Agri Connect ,Shukuru Tweve amesema kuwa mradi huo unatakelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja huku lengo likiwa ni kupata vijana wabunifu wa kibiashara ambao watakuwa chachu ya kuongeza thamani ya mazao hayo na kuleta matokeo chanya katika sekta ya usindikaji.

Amesema kuwa mradi huo utaimarisha shughuli mbalimbali za kilimo biashara katika kuongeza mnyororo wa thamani mazao ya mbogamboga na matunda lishe katika suala zima la usindikaji kwa kutumia nishati ya jua ,usafirishaji, usambazaji, ufumbuzi ,utatuzi wa kidigitali na mifumo ya utunzaji wa mbolea za asili.

“Tunaangalia zaidi eneo la ubunifu wa mifumo ya uzalishaji na usambazaji hususan katika suala zima la kilimo cha bustani za mbogamboga na matunda katika mikoa mitano lengo ni kupata ubunifu wenye tija,kuleta matokeo na kuokoa upotevu wa vyakula lishe shambani na ukosefu wa masoko,”amesema Tweve na kuongeza kuwa

“Tunashuhudia ukosefu wa teknolojia za kisasa za utunzaji wa mbogamboga na matunda ambao unachangia wakulima kupata hasara pindi anapoingiza sokoni lakini endapo vijana wakawa wabunifu itasaidia sana kupata mbadala wa kutumia teknolojia za usindikaji kwa kuongeza thamani ya bidhaa husika,”.

Tweve amebainisha kuwa vijana watakao wasilisha kazi zao za ubunifu zenye tija watapelekwa katika hatua nyingine ambayo zitaboreshwa na kuwezeshwa upatikanaji wa mitaji na vifaa vya teknolojia za kisasa ili kujiendeleza na kuwa na mitaji endelevu.

“Tulipokea jumla ya vijana 300 katika Mikoa ya Mbeya ,Iringa ,Songwe ,Katavi na Katavi waliomba kushiriki mafunzo ambapo kati yao 150 watachaguliwa kulingana ubunifu utakao pitiwa na kuchunjwa watapata fedha kati ya milioni 6 mpaka 9 milioni kwa lengo kuwekeza kwenye miradi yao,”amesema.

Mjasiriamali na mtengenezaji wa sabuni Amini Mulungu amesema kutokana na elimu ya teknolojia bunifu walizopata atapanua wigo mpana ambao utaleta matokeo mazuri kwa taifa endapo wazo la ubunifu alilowasilisha atapata uwezeshwaji kupitia mradi Agri Connect kwa ufadhiri wa Umoja wa Ulaya (EU).

“Nimefanya ubunifu wa utengenezaji wa sabuni kwa kutumia mafuta ya mawese lakini kupitia elimu niliyopata nimeona nina wigo mpana wa kutumia matunda kutengeneza rasilimali hiyo ambayo pia ni lishe kwa binadamu, ”amesema.

Naye Msindikaji Adilifestor Panja ,amesema kupitia mradi wa Agri Connect anakwenda kuongeza ubunifu ambao utaleta matokeo mazuri kwa taifa kuondokana na changamoto za masoko ya bidhaa za mbogamboga hususani kupanua wigo wa masoko ya nje ya nchi.

Kupitia mradi wa Agri connect na kutekelezwa na baadhi ya Taasisi ikiwepo Rikolto ambao utawanufaisha vijana 150 kati ya 300 watakao ingia kwenye shindano la ubunifu wa mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa chakula na utatuzi wa changamoto za kibiashara zitakazoleta mwarobaini wa upotevu wa mazao ya mbogamboga na matunda.