March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana 135 wapatiwa chanjo saratani ya kizazi Karatu

Na Sophia Fundi, Timesmajira, Karatu

ZAIDI ya vijana 135, wa kike na wa kiume wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 kutoka kata ya Daa, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, wamepatiwa huduma jumuishi ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.

Hizo ni jitihada za kuboresha upatikanaji wa huduma za kinga kwa vijana wa rika balehe.

Huduma hizo jumuishi zilihusisha utoaji wa elimu ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia, upimaji wa macho, upimaji wa hali ya lishe, pamoja na chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana ambao hawakuchanjwa awali.

Lengo ni kuwafikia vijana wote katika jamii kwa wakati mmoja na kuongeza uchanjaji wa chanjo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana.

Zoezi hilo limeratibiwa na kusimamiwa na Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa ushirikiano wa karibu na shirika la Jhpiego, kwa ufadhili kutoka GAVI – taasisi ya kimataifa inayosaidia upatikanaji wa chanjo kwa nchi zinazoendelea.

Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo, Mkurugenzi wa Mradi wa SHARP kutoka Jhpiego, Dkt. MaryRose Giattas, amesema lengo kuu ni kufikia watoto walioko nje ya shule, kwani walioko shuleni ni rahisi kuwafikia kupitia mfumo wa elimu.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuhusisha vijana wa kiume ili wapate elimu ya afya ya uzazi na namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia, jambo linalowasaidia kujitambua na kufanya maamuzi sahihi.

“Mradi huu kwa sasa uko katika hatua ya utafiti, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili – MUHAS ili kutathmini njia bora za kuwafikia watoto walioko nje ya mfumo wa shule.

“Kwa sasa tumeanza na Kata ya Daa na vijiji vyake pamoja na Kata ya Itambo mkoani Mbeya, lakini lengo ni kufikia watoto wote nchini,” amesema Dkt.MaryRose.

Kwa upande wake, Meneja wa Chanjo Taifa, Florian Tinuga, amewahimiza wazazi na walezi kutowaficha watoto wao bali wawe sehemu ya zoezi hilo muhimu la kinga na elimu ya afya.

“Huduma hii inawahusu vijana wa kike na wa kiume. Ushirikiano wa wazazi ni muhimu kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya afya,” amesisitiza Tinuga.

Zoezi hilo linaendelea kutolewa katika shule na jamii za Kata ya Daa, likiwa ni mfano wa jinsi huduma za afya zinavyoweza kuifikia jamii kwa usawa na wakati.

Mganga mkuu wa wilaya Karatu, Dkt. Hamisi Abdullah amesema ni jambo la faraja na upendeleo kwa wilaya hiyo kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wilaya mbili kufanyika kwa zoezi hilo.

“Naishukuru Wizara ya Afya,TAMISEMI pamoja na Mdau Jhpiego kwa kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya wa kata ya Daa na Kisha kuwepo kwa zoezi hili la utoaji wa hizi huduma jumuishi za chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa vijana umri kuanzia 9-14 wote wa kike na kiume hususani hawa walio nnje ya shule,” amesema.

Amesema, kama wilaya ya karatu na Kata ya Daa zitaendeleza hili zoezi kwa kutoa hii elimu ya uwepo na namna ya utoaji huduma jumuishi za chanjo kwa Kata zingine hapa Karatu, itawafikia vijana wengi zaidi.