November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vifua Viwili sasa kuwania ubingwa wa Dunia wa IBF

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

BONDIA Mtanzania anayefanya vizuri nchini Australia, Bruno Tarimo ‘Vifua Viwili’ amefanikiwa kupanda hadi nafasi ya sita katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Ngumi la Kimataifa la IBF kwenye uzito wa Super Featherweight (kg 59).

Kupada kwake hadi nafasi ya sita sasa kunamuwezesha bondia huyo kucheza mapambano ya kuwania ubingwa wa dunia wa IBF.

Akizungumza naTimesMajira, bondia huyo amesema kuwa, kitendo cha kupanda hadi katika nafasi hiyo kinampa zaidi nguvu ya kupambana kwani anachomani ni kuona ni siku moja akiwania na kushinda mkanda huo mkubwa mkubwa.

Lakini pia jambo hilo linamuongezea morali zaidi ya kufanya mazoezi ili kuweza kupambana na kuendelea kufanya vizuri kuelekea kwenye mapambano mengine yatakayokuja mbele yake katika siku za usoni na kuendelea kuweka rekodi bora zaidi.

Amesema kuwa, baada ya kufanikiwa kutetea ubingwa wake wa kimataifa ya IBF na kutwaa pia ule wa IBO alizidi kupata morali ya kuendelea kufanya vizuri ili kupanda zaidi katika viwango vya mabondia bora duniani.

Aprili 21 bondia huyo alizichapa na bondia kutoka nchini humo, Kye MacKenzie katika pambano la raundi 10 la uzani wa ‘Super Feather’ lililofanyika kwenye ukumbi wa WIN Entertainment Centre, Wollongong, New South Wales, Australia na kutwaa ubingwa baada ya majaji wawili kumpa alama 97-93 kila mmoja na jaji wa tatu alimpa Bruno alama 94 dhidi ya 96 za mpinzani wake.

“Nashukuru Mungu kwa kufanikiwa kupanda hadi kwenye nafasi hii kwani nilikuwa nikihitaji sanakushinda kila pambano lililo mbeye yangu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi katika orodha ya mabondia bora ulimwenguni na sasa nashukuru hili limetimia,” alisema Bruno.

Itakumbukwa kuwa, Desemba mwaka jana bondia huyo alifanikiwa kutwaaWorld Boxing Association Oceania na International Boxing Federation International katika pambano lililomalizika kwa sare dhidi ya bondia Paul Fleming wa Australia.

Vifua Viwili alitetea ubingwa huo wa IBF ‘IBF International Super Feather Weight’ baada ya kumshinda kwa pointi mpinzani wake, Nathaniel May katika pambano litakalofanyika Desemba 6, 2019 katika pambano lililofanyika katika mji wa Sydney nchini Austraria.

Ubingwa huo wa IBF aliutwaa baada ya kumpiga kwa pointi bondia wa Serbia, Serif Seka Gurdijeljac katika pambano la raundi 10 lililofanyika Agosti 31 kwenye ukumbi wa Hala Pendik Novi Pazar kuendelea kuweka rekodi nzuri katika mchezo huo.

Katika pambano hilo, kwa mara ya kwanza Vifua viwili alivunja rekodi ya bondia huyo mwenye umri wa 32 ambaye hajawahi kupigwa wala kupata sare katika mapambano 26 aliyoyacheza.

Mwamuzi wa pambano hilo, Will Soulos alitangaza pambano hilo kutokuwa na bingwa baada ya majaji kutoa alama zinazofanana mabondia hao.