January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Picha ya Aljazera

Vifo vya COVID-19 vyafikia 200,000

GENEVA, Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kuwa, idadi ya vifo duniani kutokana na janga la virusi vya corona (COVID-19) ni zaidi ya 200,000.

Mbali na hayo limebainisha kuna umuhimu wa kutolewa vibali maalum kwa watu waliopona ugonjwa wa COVID-19.

Rekodi ya hali ilivyo Duniani kuhusu maambukizo, vifo na waliopona leo tarehe 27/04/2020 Jumatatu saa 08:23

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO ilieleza kuwa,hakuna ushahidi kuwa mtu aliyepona hawezi tena kuambukizwa virusi vya corona.

Mbali na hayo pia WHO imeonya bado hakuna uthibitisho kuwa wagonjwa waliotengamaa wana kinga ya mwili kuzuia kupata tena maambukizi na kusisitiza nadharia hiyo inahitaji tathmini zaidi.

Mataifa kadhaa yamezungumzia fikra hiyo, kwamba wale waliopatikana na kinga ya mwili dhidi ya virusi vya corona wanaweza kurejea haraka kazini na katika maisha ya kawaida.

Jumla ya visa vya maambukizi ya ugonjwa huo duniani imepanda hadi watu milioni 2.86. Aidha, nchini Marekani, idadi ya vifo imepanda na kufikia watu 53,511.

Mbali na hayo, Kundi la nchi 20 tajiri na zinazoinukia kiuchumi duniani la G20 limezindua mpango wa kimataifa wa kuharakisha upatikanaji wa vifaa vya kiafya vinavyohitajika kupambana na virusi vya corona.

Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia, ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa G20, Mohammed al-Jadaan alisema kundi hilo bado linajitahidi kuziba pengo la ufadhili wa takribani dola bilioni nane wa kupambana na janga hilo.

Aliongeza kuwa, jamii ya kimataifa bado inakabiliwa na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu ukubwa na muda ambao janga hili la kiafya litatatuliwa.

Mapema mwezi huu, Serikali ya Saudi Arabia iliahidi dola milioni 500 za kuunga mkono juhudi za kimataifa za kupambana na janga la virisi vya corona.