Na Mwandishi Maalum,WAMJW – Mwanza
VITUO vya kutolea huduma za afya nchini vimetakiwa kufanya uchunguzi wa kifo chochote kitakachotokana na ugonjwa wa Corona ili kubaini kama mgonjwa alihudumiwa ipasavyo kabla ya kifo kutokea.
Agizo hilo limetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi, akiwa Jijini Mwanza mara baada ya kuagana na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa – Bugando alipokuwa akifanya kazi awali kama Mkurugenzi Mtendaji kabla ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
“Kwa kweli tusingependa kuona mgonjwa anafariki kwa sababu zisizo na msingi, naagiza hospitali zote zenye kamati ya uchunguzi (Clinical Audit) kufanya uchunguzi wa vifo vinavyohusiana au kutokana na corona ili kuona kama kulikuwa na tatizo lolote katika kumpokea mgonjwa au katika kumhudumia,” amesema Prof. Makubi
Prof. Makubi amewataka wananchi kuelewa kuwa sio kila kifo kinachotokea hivi sasa kinasababishwa na ugonjwa wa Corona kwa kuwa yapo magonjwa mengine pia ambayo yanatushambulia binadamu.
“Siyo kweli kwamba mgonjwa akiwa na presha, kisukari, figo au kansa akifariki iwe imesababishwa na corona, tuendelee kuwahudumia wananchi, kuepusha vifo vinavyoweza kuwa na uhusiano wa Corona,” amesema Prof. Makubi.
Aidha, Prof. Makubi ametoa rai kwa vituo vya afya kuwapokea wagonjwa wote na kuwapatia matibabu bila kuwabagua kuwa na dalili za corona.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria