November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vifaa vya kujipima Ukimwi kupungua bei

GENEVA, Shirika la Kimataifa la Kufanikisha Uwepo wa Tiba Nafuu Duniani (UNITAID) ambalo linaratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ongezeko la upatikanaji katika soko na kushuka kwa bei kwa asilimia 50 kwa vifaa vinavyotumiwa na mtu binafsi kujipima iwapo ana Virusi Vya Ukimwi (VVU) au hana.

Kwa mujibu wa shirika hilo, hatua hiyo inafuatia makubaliano na kampuni binafsi ya Viatris kupitia kampuni mama ya Mylan ambapo kuanzia sasa makasha ya kujipima VVU yanayotumia damu yatauzwa kwa chini ya dola mbili kila kimoja katika nchi 135 zinazokidhi vigezo duniani.

Msemaji wa UNITAID, Herve Verhoosel amesema,kitendo cha mtu kupata vifaa vya kujichunguza mwenyewe VVU kimetambuliwa kuwa kigezo muhimu katika kufikia lengo la kimataifa la asilimia 90 ya watu kufahamu iwapo wameambukizwa VVU au la.

“Katika kipindi cha miaka sita iliyopita,kiwango hicho cha kutambua hali ya VVU kwa mtu kilikuwa kimeongezeka kutoka asilimia 45 hadi 81,”amesema.