Na Joyce Ksiki,Timesmajira online,Mbeya
JAMII imeaswa kutowadharau na kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum wakiamini kwamba hawawezi kitu chochote.
Mwalimu wa Chuo cha Ufundi (VETA) Chang’ombe jijini Dar es Salaam Kintu Kilanga ameyasema hayo katika maonyesho ya wakulima Nane nane yanayoendelea jijini Mbeya .
Amesema,watoto hao wanahitaji kupata haki zote za msingi kama wanazopata watoto wengine kama vile elimu,afya na mahitaji yote muhimu anayostahili kupata mtoto yeyote na siyo kuwafungia ndani.
“Jamii imekuwa ikiwatazama watoto wa kundi la mahitaji maalum kama watoto wasiojiweza kwa kitu chochote jambo hili siyo sahihi,hawa watoto pamoja na changamoto waliyo nayo,lakini wana uwezo mkubwa na wanafundishika japo uelewa wao ni wa taratibu.”amesema Kilanga
Amesema katika darasa lake anawafundisha watoto wenye mahitaji maalum wapatao 23 kozi ya kuunga vyuma (kuchomelea) na wanafanya vizuri na kwa kushirikiana na wanafunzi wanatengeneza mashine rahisi ya kupukuchua mahindi.
Kilanga amesema,wametengeza mashine hizo baadhi tayari wameshawauzia wateja na baadhi ya mashine wamekwenda nazo kwenye maonyesho ya Nane Nane kwa ajili ya kuwaonyesha wakulima na wananchi kwa ujumla mashine hizo zinazorahisisha kazi na kuyaweka mazao katika usalama wa chakula.
Mmoja wa wanafunzi hao Mohamed Selemani ambaye sasa ni fundi kuchomelea amesema,anafurahia kushiriki kwenye maonyesho akiwa na mashine waliyoitengeneza wao wenyewe licha ya kuwa jamii imekuwa ikiwadharau.
“Jamii iwawezeshe watoto wenye mahitaji maalum,na sisi tunaweza kufanya vitu kama wanavyoweza watoto wengine,hii inatusaidia kujitegemea kiuchumi.”amesema Mohamed
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja