March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA yatakiwa kuwa chachu ya Mapinduzi ya viwanda

Na Joyce Kasiki,Timesmajira pnline,Dodoma

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Profesa Sifuni Mchome, ametembelea banda la VETA katika maonesho ya kilimo ya Nanenane ya Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.

Katika ziara hiyo, Profesa Mchome alishuhudia ubunifu na teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na vijana wa vyuo vya VETA kutoka maeneo tofauti nchini huku akionyesha kufurahishwa na hatua kubwa ambazo taasisi hiyo imepiga katika kuendeleza ubunifu unaohusiana na matumizi ya nishati jadidifu kama jua na maji, pamoja na teknolojia rafiki kwa wakulima na jamii kwa ujumla.

Profesa Mchome alitembelea maeneo mbalimbali ya banda hilo na kujionea mashine ya kumwagilia inayotumia nishati ya jua, vifaa vya kutengeneza chakula cha mifugo kama kuku, pamoja na mavazi ya kisasa yaliyobuniwa na wanafunzi wa VETA.

Katika hotuba yake kwa waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, Profesa Mchome alisisitiza umuhimu wa kubadilisha bunifu hizo kuwa bidhaa za viwandani zitakazoenda jadi kwenye soko ili ziweze kutatua changamoto katika jamii.

“Sasa ni wakati wa kuingia kwenye uzalishaji mkubwa. Vifaa hivi vina tija kubwa, vinaweza kusaidia wakulima wetu, wafugaji, na hata sekta nyingine. Tunapaswa kuhakikisha vinazalishwa kwa wingi na kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.”amesema Prof.Mchome

Aidha, amesisitiza kuwa VETA ina nafasi kubwa ya kuchangia katika kufikia dira ya maendeleo ya taifa, hasa kupitia uzalishaji wa teknolojia bunifu zitakazotatua changamoto za kila siku za wananchi.

Katika maonesho hayo, VETA imeonyesha uwezo wake wa kutoa ujuzi wenye tija, na imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha vijana wanajifunza si tu kwa nadharia, bali pia kupitia utekelezaji wa vitendo na ubunifu unaogusa jamii.