Judith Ferdinand
Waswahili wanasema uchungu wa mwana,aujuae mzazi,na utamu wa ngoma uingie ucheze,msemo huu umejidhihirisha kwa Valentina Enos,mkazi wa Kisiwa cha Bezi kilichopo Kata ya Kayenze, wilayani Ilemela mkoani Mwanza,ambaye amenusurika na kifo na kujikuta akipoteza mtoto na kuambulia kovu la maisha tumboni.
Hii yote ni kutokana na kukosekana kwa kituo cha kutolea huduma za afya kisiwani humo hali inayowapa wakati mgumu wajawazito,ambao wanajikuta wakipoteza matumaini ya uhai pindi wanaposhikwa na uchungu.
Hata hivyo Serikali na wananchi hawakukaa kimya walianza jitihada za ujenzi wa zahanati ambayo bado haujakamilika.Nami sikusita kujionea ujenzi huo wa zahanati na baada ya hapo natembea nusu kilomita mpaka nyumbani kwa Valentina Enos mama wa watoto watano,nikiongozwa na mwenyeji wangu Mjumbe wa Serikali ya mtaa wa Bezi, Esther Warioba.
Tunabisha hodi na kupokelewa na Valentina,na baada ya utambulisho mazungumzo yetu yanaanza hivi,”Sitasahau siku ya Juni 28,2025,laiti zahanati ingekuwepo nisinge teseka wala kupata kovu na mtoto wangu angekuwa hai mpaka sasa,”anasema.
Valentina anasema,yeye ni mama wa watoto watano kwa sasa ambao wapo hai,akiwa na nzao nane ambapo watoto wawili walifariki mmoja akiwa na miaka minne na mwingine miaka miwili huku nzao mmoja ndiye msingi wa simulizi hii ambaye alizaliwa akiwa ameisha fariki.
Kipindi cha ujauzito hali ilikuwaje
Valentina,anasema katika maisha yake hajawai kutumia njia ya uzazi wa mpango licha ya kuwa na nzao nane, na kipindi cha ujauzito hakuwai kuwa na changamoto yoyote ya kiafya au mimba kuwa na viashiria vya hatari.Na alikuwa akifanya shughuli zake kama kawaida akisubilia siku ya kuleta kiumbe kipya duniani ifike.
Anasema,licha ya huduma za afya kutokuwepo kisiwani humo lakini alijitahidi kuhudhuria kliniki kipindi chote cha ujauzito katika kituo cha afya Kayenze.
Ambapo ili afike huko alitumia takribani saa moja na dakika 20 akiwa majini kwa usafiri wa kivuko cha Mv.Ilemela,na akifika gati la Kayenze analazimika kutembea kwa miguu kwa takribani dakika 20 ili kufikia huduma za afya katika kituo cha afya Kayenze.
“Licha ya huduma za afya kuwa mbali lakini nilikuwa nahudhuria kliniki kama kawaida,napata vipimo vyote kutoka kwa wahudumu wa afya,na walikuwa wakinieleza kuwa sina changamoto yoyote,”anasema Valentina.
Safari ya kujifungua
Valentina anasimulia kuwa,ilikuwa Jumamosi ya Juni 28,2025, asubuhi kwenye saa tatu ndipo uchungu ulianza kumuuma na wakati huo kivuko cha Mv.Ilemela kilikuwa kimeisha ondoka kuelekea Kayenze,kwani kinafanya kazi kwa muda maalumu na alikuwa ana fedha za kukodi mtumbwi kiasi cha laki moja (100,000).
“Wakati huo mme wangu hakuwepo,nilihangaika na uchungu huku nikivumilia na kutulia ili ikiwezekana nijifungulie nyumbani au ikifika saa nane mchana bado sijajifungua,muda ambao kivuko kitatoka kisiwani Bezi kwenda Kayenze basi nivuke maji na kufika kituo cha afya Kayenze,”anasema Valentina.
Anasimulia kuwa,baada ya kupita saa moja uchungu ulizidi kuwa mkali na kuhisi kutaka kusukuma ili mtoto atoke,hivyo aliingia ndani na kuanza kuhangaika kusukuma lakini mtoto hakutoka.
Hivyo ilibidi kufanya jitihada za kumuita jirani ambaye alifika na kumkuta Valentina akiwa ndani anahangaika kusukuma na kulingana na hali alijitahidi bila mafanikio.
‘Baada ya kusukuma bila mafanikio nikamuomba jirani yangu amfuate Daktari ( muuzaji wa duka la dawa kisiwani hapo), alivyofika akanipima njia na kuniambia ipo sawa,akasema ngoja afuate vifaa,alivyoondoka nikaona kama anachelewa kurudi wakati huo uchungu ulizidi kuchanganya,”anasimulia.
Anasema,mara chache uwa inakuja meli ya matibabu ya wachina kisiwani humo kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa wananchi na siku hiyo ilikua bahati kwa sababu meli hiyo ilikuwa imetia nanga kwenye Gati la Bezi.
Baada ya kuona muuzaji wa duka la dawa amechelewa alimtuma tena jirani aliyemsaidia kwenda kwa wachina hao,ambaye aliwafuata na kuja na mmoja wa madaktari wanaotoa huduma kwenye meli hiyo.
“Muda mfupi jirani alirejea akiwa na Daktari kutoka kwenye meli hiyo ya matibabu,ambaye alifika na kuniwekea chupa(dripu) ya maji ya uchungu,nayo iliisha lakini hakukuwa na mafanikio yoyote,”anasimulia Valentina na kuongeza:
“Ikabidi wanibebe na kunipeleka kwenye meli wanapotolea huduma za matibabu eneo la gati la Bezi,na baada ya kuniingiza ndani ya meli wakanipima na kusema uwezekano wa mimi kujifungua kawaida haupo inabidi nifanyiwe upasuaji na wao hawana vifaa kwa ajili ya zoezi hilo,”anasema Valentina.
Safari ya kuokoa maisha yake na mtoto
Valentina anasema,baada ya wataalam wa meli ya kichina kubaini kuwa siwezi kujifungua kawaida na wao hawana vifaa,walishauriana kunipeleke kituo cha afya Sangabuye.
“Wakanichukua na kuniweka kwenye boti yao ya mwendo kasi na kunifikisha mpaka kituo cha afya Sangabuye,tuliwakuta madaktari tayari wapo mwaloni kwani waliwapigia simu,kisha wakanibeba na kunifikisha kwenye chumba cha huduma na kunipima tena,”anasema.
Anasimulia kuwa wakati huo alikuwa hawezi kuzungumza wala kufanya jambo lolote kwa sababu uchungu ulikuwa mkali zaidi na maumivu yalikuwa yanaongezeka ingawa alikuwa anasikia na kuona.
“Wakaniuliza tukufanyie upasuaji,nikawa nakubali kwa kichwa,sikuweza kuweka saini,hivyo Daktari akasaini kwa niaba yangu na mme wangu kwa sababu wakati huo sikuweza kufanya chochote,”anasimulia Valentina na kuongeza:
“Wakaniingiza kwenye chumba cha upasuaji na walifanikiwa kunifanyia upasuaji na kumtoa mtoto ambaye tayari alikuwa ameisha fariki, na baada ya hapo nikatolewa na kupelekwa wodini kuendelea na huduma nyingine nikiuguza kidonda na hiyo ndio ilikuwa pona pona yangu,”.
Haya hivyo anasema endapo kungekuwa na hospitali au kituo cha kutolea huduma za afya pengine yeye na mtoto wangenusurika.
“Yote yametokea kwa sababu huduma ilikuwa mbali.Namshukuru Mungu nimenusurika lakini mtoto nimekosa lakini pia kizazi kimefungwa hivyo sitarajii kupata mtoto tena kwa sasa,”anasema.
Kauli hii inaungwa mkono na Mwenyekiti wa mtaa wa Kisiwa cha Bezi, James John,anayesimulia namna jitihada zilizofanya na Daktari anayetoa huduma kupitia meli alivyoweza kuokoa maisha ya mama huyo licha ya mtoto kufariki.
John,anasema,wajawazito kisiwani humo wanawasumbua sana hususani viongozi,mama mjamzito akiumwa uchungu hata saa saba za usiku,lazima Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa agongewe hodi au Mjumbe wake ili angalau wamtafutie usafiri wa kumpeleka kwenye huduma.
Anasema,jitihada za kutafuta usafiri wa kumuwahisha mama huyo kwenye kituo cha huduma, wanaweza kutumia zaidi ya saa sita na hatari kwa mama na mtoto ipo zaidi pale ukikuta kuna tatizo la kukosa usafiri wakati huo au fedha za kukodi mtumbwi hazipo.
“Tumeisha wahi kupitia majanga haya ya mama kupoteza maisha pamoja na mtoto wakati wa kujifungua au akiumwa uchungu,kuna watu walipoteza maisha kwa kukosa huduma ya uzazi.Pia juzi juzi tu hapa mradi wa ujenzi wa zahanati ukiwa unaendelea kuna mama mjamzito alinusurika kupoteza maisha lakini mtoto alifariki,”anasema John.
John anasisitiza kuwa,kilichowasaidia mama akanusurika wakati anaumwa uchungu kulikuwa na meli ya matibabu ambayo utoa huduma ya afya kisiwani hapo kila baada ya miezi sita hadi saba.
Hivyo siku hiyo meli hiyo ilikuwa kisiwani humo na baada ya mama huyo kuumwa uchungu na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha,wataalamu wa afya walimbeba kwenye boti ya mwendo kasi na kumkimbiza kituo cha afya Sangabuye ambacho kipo Kata jirani.
“Walivyomfikisha kituo cha afya Sangabuye kwa taarifa nilizopewa na Daktari Mkuu wa meli hiyo, madaktari wa kituo hicho walimktaa ila yeye alijaribu kuomba ili amuhudumie,na kama bahati nasibu na kwa uwezo wake daktari huyo akamsaidia mama huyo kwa kuokoa uhai wake lakini mtoto alikuwa tayari ameisha fariki,”anasema John.
Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya mtaa wa Kisiwa cha Bezi, Esther Warioba,anasema,wapo wanawake wengi ambao wamepoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na kukosa huduma za afya kisiwani humo.
“Kipo kisa cha dada mmoja mke wa Kaliwa(Valentina Enos),aliumwa uchungu ghafla,wakati tunajianda ili tumkimbize katika kituo cha afya Sangabuye tayari mtoto alikuwa ameisha shuka, bahati kulikuwa na boti fulani ya wachina ambayo uwa inakuja huku mara moja moja kutoa huduma za afya,ndio ikamkimbiza na kumfikisha katika kituo cha afya,”anasema Esther na kuongeza:
“Ikabidi wamfanyie upasuaji wakakuta mtoto tayari ameisha fariki tukio hilo limetokea kama miezi miwili iliopita na vifo vingine vingi vya wakina mama na watoto,ambao wengine siwajui majina maana yake humu kisiwani tunaingia na kutoka,hali ambayo inatupa wasiwasi,”.
Anasema,wameteseka sana na kuhangaika wamama wajawazito,mtu akibeba mimba anaanza kuwaza kuanzia ujauzito una mwezi mmoja mpaka miezi tisa,”sijui nitakufa,sijui sita kufa,Mungu anasaidie wengine wanapona wengine wanafariki,”
“Kati ya mwaka jana au juzi,kuna mama mwenzetu alipoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma na msaada wakati wa kujifungua.Wanawake tulijitahidi huku na huku kumnusuru yeye na mtoto wake lakini jitihada zetu hazikuzaa matunda mama yule na mtoto wake walipoteza maisha,”anasema Esther.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Dkt.Maria Kapinga,anasema idadi ya vifo vya uzazi vilivyoripotiwa katika Kisiwa cha Bezi kwa kipindi cha 2020–2025 ni vifo viwili ambapo mwaka 2020 hakuna kifo,2021 kifo kimoja,2022 kifo 0,2023 kifo 1, kilichotokea kwenye jamii(community death),2024 kifo 0 na 2025 kifo
0.
Dkt.Kapinga, anasema,Kisiwa cha Bezi hakina zahanati na wananchi hutegemea huduma kutoka kwa wahudumu wa afya wa kujitolea au kusafiri kwenda Sangabuye au Kayenze kupata huduma za afya ikiwemo huduma za afya ya
uzazi.
“Tunategemea madaktari wa maduka ya dawa hapa kisiwani Bezi,kutusaidia wakati wa kujifungua,natamani zahanati hii ikamilike kwa haraka kwani humu wajawazito ni wengi,madaktari wawe karibu,vifaa tiba viwepo vya kutosha ili kuokoa maisha ya mama na mtoto,”anasisitiza Valentina Enos.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama