December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uzinduzi wa Ofisi ya TOST mwanzo wa migogoro ya kodi kusuluhishwa kwa wakati

Na Reuben Kagaruki,Timesmajira Online,Dar

KWA muda mrefu kumekuwepo migogoro ya kikodi baina ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Migogoro hiyo imekuwa ikisababisha mvutano baina ya wafanyabiashara na TRA, huku wafanyabiashara wakidai kutotendewa haki.

Aidha, kwa nyakati tofauti tumemshuhudia Rais Samia Suluhu Hassan akikemea ukusanyaji wa kodi kwa kutumia nguvu na mabavu, akisema hausaidii, umesababisha wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao kwa kuhofia kubambikiwa kesi.

Pamoja na maelekezo hayo, katika uongozi wake, Rais Samia, ameweka msisitizo wa ulipaji wa kodi unaolenga kusimamiwa kwa haki.

Amekuwa akisisitiza hilo na kwamba uongozi wake umejitaidi kuweka mazingira mazuri zaidi ya kufanya biashara nchini.

Kwa kudhihirisha hilo, Serikali imeunda Taasisi ya Usuluhuhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman Service of Tanzania TOST) ikiwa ni taasisi huru ya usuluhuhishi na malalamiko ya taarifa za kodi.

Akizungumza wakati na uzinduzi wa ofisi ya TOST Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba Madelu, ameiagiza Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi (TOST) kuhakikisha inatatua migogoro mbalimbali ya kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kukusanya mapato pamoja na kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Dkt. Nchemba ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Ofisi hiyo mpya ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha.

Dkt. Nchemba anasema kuwa Serikali inatarajia kwamba Ofisi hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya kikodi na kuongeza kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari, hivyo kuongeza mapato ya Serikali.

“Ofisi hii utasaidie kupunguza migogoro ya kodi na kuongeza kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari, siku tukifanikiwa kuongeza idadi ya walipakodi (taxbase), tutakuwa na uhuru mkubwa sana wa kupunguza hivi viwango vya ulipaji kodi”, anasema Dkt. Nchemba.

Anasema ni matarajio ya Serikali kuwa ustawi wa biashara utaongezeka kutokana na walipa kodi kupata jukwaa huru litakalotoa fursa ya kusikiliza changamoto zinazohusu usimamizi wa sheria ya kodi pamoja na huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Anasema Wizara ya Fedha itaendelea kusimamia na kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo kwa kuhakikisha kuwa mahitaji yote muhimu yanapatikana ikiwemo rasilimali watu, vifaa na mifumo ya kisasa ili iweze kutoa huduma bora kwa walipa kodi.

Aidha, Anaagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kukusanya kodi kwa weledi kwa kutafuta njia ya majadiliano na wafanyabiashara wanaokiuka taratibu badala ya kufunga biashara zao.

Dkt. Nchemba anawaagiza Wafanayabiashara kufanya biashara zao kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kuepusha misuguano isiyo ya lazima na Mamlaka ya Mapato.

Pia anatoa rai kwa wananchi kuwa wazalendo kwa kulipa kodi stahiki na kwa wakati, kudai risiti halali kulingana na kiwango cha fedha walichotoa na wafanyabiashara kufanya matumizi sahihi ya mshine za kutolea risiti kwa njia ya kielekroniki (EFDs) pamoja na kutoa risti halali kwa wateja wao.

“Watu wanaostahili kutumia mashine za EFDs watumie, kutokufanya hivyo ni kujitafutia matatizo wenyewe. Kutokutoa risiti na kusingizia mifumo sio suluhisho la kudumu, huku ni kuahirisha matatizo” alisitiza Mhe. Dkt. Nchemba.

Anasema kufanya hivyo, kutaiwezesha Serikali kutoa huduma muhimu za kijamii ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali itakayoboresha maisha yao na kupunguza umasikini ikiwemo maji, elimu, miundombinu wezeshi kiuchumi na mambo mengine mengi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Usuhulishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Robert Manyama anasema kuwa Taasisi yake imejipanga kutatua changamoto za taarifa za kikodi za wananchi katika ubora wa hali ya juu kwa kuwa imeweka mazingira rafiki na rahisi ya wananchi kuwasilisha malalamiko yao popote walipo pamoja na kuwa na wafanyakazi wenye ueledi na waliotayari kutoa huduma kwa walipa kodi.

“Kipaumbele cha Ofisi hii ni kuhakikisha kwamba malalamiko yote yanashughulikiwa kwa uhuru kamili, haraka, haki na usawa”, alibainisha.

Anasema Ofisi hiyo imeanzishwa kutokana na marekebisho ya Sheria ya Fedha namba 8 ya mwaka 2019, yaliyosababisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi SURA 438, kwa kuongeza sehemu ya IIIA – Uanzishaji wa Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Establishment of Tax Ombudsman office.)

Akizungumza hivi karibuni na na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika ukumbi wa Hazina Ndogo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuitambulisha Ofisi hiyo pamoja na malengo na wajukumu ya kuundwa kwa Taasisi hiyo huru ya Usuluhishi, Manyama, anasema;

“Taasisi hii inafanya shughuli zake kwa ufanisi na tumetoa fursa hii kuwajulisha wananchi kuhusu taasisi hii na majukumu yake,” anasema Manyama.

Anasema kuundwa kwa TOST kunatokana na nia nje ya Serikali na Bunge kwa pamoja kuridhia kuanzishwa kwa ofisi huru yenye mamlaka ya kisheria kushughulikia malalamiko ya walipa kodi yanayotokana na taratibu, huduma au maamuzi yanayotokea kwa usimamizi wa sheria ya kodi unaofanywa na TRA.

Anasema Ofisi ya TOST imeanzishwa chini ya sheria iliiyounda taasisi hiyo.

Anasema ilianzishwa mwaka 2019 kwa marekebisho yaliyofanywa katika Sheria ya Usimamizi wa Kodi, 2015: Sura ya 438 kwa kuongeza sehemu ya 11A yenye vifungu vya 28A hadi 28F.

Anasema ujenzi wa taasisi na mifumo yake ulianza Februali 2023 baada ya Waziri wa Fedha kutengeneza kanuni zilizochapishwa katika gazeti la Serikali, GN 105 na GN 106.

Anasema tayari Serikali imehamishia watumishi jijini Dodoma na kuunda taasisi chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha. Kwa mujibu wa Manyama taasisi inaendelea kujiimarisha na sasa iko tayari kutoa huduma kwa jamii kwa kupokea malalamiko yaliyopo yatokanayo na maamuzi yasiyoridhisha au taratibu zisizokubalika za kutoza kodi.

Manyama anasema mambo hayo matatu yanatokana na usimamizi wa sheria ambazo zinasimamiwa na TRA.

Anafafanua kuwa TOST na TRA ni taasisi mbili huru za Serikali, zilizohundwa na kupewa majukumu matatu. Moja kuhakikisha mfumo wa kodi nchini unatoa huduma kwa ufanisi na kwa kuongeza ulipaji wa kodi.

Anafafanua kwamba kwa sasa TOST ina ofisi jijini Dodoma na ina mpango wa kuwa na ofisi nyingine jijini Dar es Salaam.

Kuhusu madhumuni ya kuundwa kwa taasisi, Manyama anasema ni kama ifutavyo;

Moja, kushughulikia malalamiko yatokanayo na sheria za kodi zinazosimamiwa na TRA, kwa kanuni, ufanisi, uwazi, uhalisia na usiri wa taarifa za wafanyabiashara.

“Kwa hiyo taasisi inashughulikia malalamiko ya kodi ikizingingatia misingi hiyo,” anasema Manyama.

Mbili, Manyama anasema taasisi ina jukumu la kuhakikisha maeneo katika usimamizi wa sheria za kodi ambayo ndiyo vyanzo vya malalamikoa kwa walipakodi nchini yanaainishwa na kutoa mapendekezo kwa Waziri wa Fedha.

Tatu, ina jukumu la kupunguza mlundikano wa kesi za kodi mahakamani na kuwezesha kupatikana kwa suluhu kwa haraka ndani ya siku 30 kwa usimamizi wa sheria za kodi.

Manyama, anasema lengo lingine ni kuhakikisha unakuwepo ulipaji wa kodi wa hiari kwa kuhakikisha taratibu na huduma za usimamizi wa kodi zinafuatwa bila unyanyasaji.

Manyama anataja aina ya malalamiko yanayoshughulikiwa na TOST kuwa ni malalamiko yote ya walipa kodi yanayotokana na utoaji wa huduma za kodi au maamuzi ya kiutawala yanayofanywa na TRA.

Kuhusu ni nani anaweza kulalamika, Manyama anasema ni mtu yoyote ambaye haridhishwi na utendaji katika maeneo tajwa, mlalamikaji anatakiwa na sheria kuwa amewasilisha malalamiko kwa msuluhishi ndani ya siku 90 tangu kutokea kwa hilo lalamiko.

Kuhusu ni nani anaweza kulalamikiwa, Manyama anasema inaweza kulalamikiwa TRA, Kamishna Mkuu wa TRA na mfanyakazi yeyote wa TRA ambaye anakiuka mambo matatu tajwa.

Anasema kwa mujibu wa Sheria ya TOST, malalamiko hayo yatashughulikiwa ndani ya siku 30 na kutoa mapendekezo yake kwa Waziri wa Fedha ndani ya siku 14.

Hata hivyo, utekelezaji huo ndani ya siku 30 unategemea huyo mlalamikaji kapeleka taarifa kuhusiana na lalamiko lake ndani ya muda gani.

Aidha, Manyama anasema taasisi hiyo hahitaji kuweka uwakilishi wa kutumia mwanasheria, mtu binafsi anaweza kuwasilisha lalamiko lake na likashughulikiwa.

Anasema taasisi hiyo inatumia zaidi majadiliano na kushirikishana kwa kuangalia uhalisia wa tatizo na sio kwa kutumia sheria, lakini sio kuvunja sheria.

“Tunaangalia tatizo kwa uhalisi wake, limetokeaje na kuona namna ya kukusaidia ili uweze kuendelea kutelekeza wajibu wako,” anasema Manyama.

Anasema katika kutekeleza majukumu yake, TOST inazingatia misingi ifuatayo, msingi wa kuanza ni kwamba ni taasisi huru , ambayo haingiliwi na taasisi nyingine wala mtu yeyote au kuzingatia maelekezo wanapokuwa wanshughulikia suala la malalamiko ya kodi.

Msingi wa pili, kuhakikisha haki za mlipa kodi na mtoza kodi zinalindwa, taasisi haiengemei upande wowote wa mlipa kodi au mtoza kodi.

Anataja msingi mwingine ni kushughulikia malalamiko kwa gharama nafuu, kwa kuondoa urasmu usioleta ufanisi.

Msingi mwingine ni kushughulikia malalamiko kwa kuangalia uhalisia mazingira ambayo yamesababisha malalamiko kutokea. Alisema taasisi hiyo ina jukumu la kutunza nyaraka na taarifa kwa usiri mkubwa, isipokuwa zitakapotakiwa kwa mujibu wa sheria.

“Hiyo ndiyo misingi inayozingatiwa katika kutenda haki,” anasema Manyama. Hata hivyo anasema taasisi haimlazimishi mtu kupeleka malalamiko hayo kwenye taasisi, bali mtu anaweza kuamua kwenda mahakamani.”
MWISHOOOOOOOOOOOOOOOOOOO