December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uzembe barabarani bado chanzo cha ajali nchini

Na Penina Malundo, Timesmajira

USALAMA barabarani ni suala mtambuka ambalo jamii inatakiwa kulitilia mkazo ili kukomesha vitendo vinavyochochea uwepo wa ajali nyingi.

Mwendokasi, unywaji wa pombe pamoja na makosa ya kibinadamu kwa asilimia kubwa yamekuwa yakichangia ajali kutokea.

Madereva wanaposhindwa kufuata sheria za usalama barabarani ni rahisi kusababisha ajali kukosekana umakini wanapoendesha magari yao.

Sera madhubuti na utekelezaji wake, miundombinu bora ya barabara na kampeni kubwa za uelewa kwa umma navyo vinaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu katika miongo ijayo.

Matukio ya ajali za barabarani yanaonekana kuanza kushika kasi ambapo ndani ya mwezi mmoja takriban watu zaidi ya 33 walipoteza maisha na wengine 82 kujeruhiwa katika ajali tatu tofauti zilizotokea Korogwe mkoani Tanga, Dodoma na Manyara.

Matukio haya ya ajali yanaonekana kujirudia kwa sababu zilezile ikiwemo uzembe wa madereva, unywaji wa vilevi pindi wakiwa wanaendesha vyombo vya moto, mwendokasi pamoja na kutopumzika wanapoendesha umbali mrefu.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya waathirika wa ajali za barabarani ni watembea kwa miguu huku asilimia 60 iliyobakia kwa watumiaji wengine wa barabara kama vile waendesha bodaboda, baiskeli na magari.

Kiongozi wa Chama cha Madereva nchini, Abdallah Lubala, anasema ajali zinapotokea zinasababishwa na mambo mengi, lakini sababu za msingi ni makosa ya kibinadamu, makosa ya kimiundombinu, vyombo vyenyewe vya usafiri, uzembe wa madereva pamoja na makosa ya wasimamizi wa sheria.

“Sababu hizi ni miongoni mwa zinazosababisha ajali kujirudi kutokana na makosa yale yale, hivyo ni vyema kila idara, ikiwemo Jeshi la Polisi, kuhakikisha kitengo cha usalama barabarani kinachukua hatua pindi wanapofanya ukaguzi wa magari kabla ya kutoka vituoni au sehemu ya mizani,” anasema.

Akitolea mfano wa ajali zilizotokea hivi karibuni, anasema magari yanapoharibika barabarani yanapaswa kutolewa kwa haraka ili yasiweze kusababisha ajali.

“Lakini nchi yetu haina vyombo ya kuyatoa yale magari yanayoharibika barabarani ambayo huwa yanasababisha ajali kwa kiasi kikubwa kutokana na muono mdogo au mshtukizo wa magari yanayopita, pengine kutokujua kama kuna gari lililoharibika. 

”Unakuta gari lina taa moja, badala ya Polisi wanaokagua magari njiani kulisimamisha na kumwambia dereva hakuna kuondoka hadi ununue taa nyingine, utakuta wao Polisi wanaliruhusu, zaidi wanampiga faini dereva, na kwa kufanya hivyo inakuwa siyo dawa kwa maana gari lile linaweza kusababisha ajali,” anasema.

Aidha, anasema kuendesha gari huku mtu akiwa amelewa ni kosa, lakini kosa linarudi kwa wakaguzi wanapokagua magari na kuwapima vilevi madereva hao na ajali inapotokea utasikia chanzo cha ajali ni pamoja na kilevi.

Kwa upande wake, Mdau wa Masuala ya Usalama Barabarani kutoka Baraza la Ushauri wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CC), Leo Ngowi, anasema mara nyingi ajali haitokei tu ila husababishwa pale dereva anapokuwa anaendesha chombo cha moto.

Anasema serikali imekuwa na mikakati mingi ya kuzuia ajali, lakini wanapoona ajali 

zinajirudia mara kwa mara, wao kama Baraza wamejaribu kutafakari kwa kina na kuona kwamba kuna vyanzo vingine vinne ambavyo havijabainishwa kwa uwazi na kufanyiwa utafiti ambavyo vimekuwa vinasababisha ajali kujirudia.

Miongoni mwa vyanzo hivyo, anasema, ni pamoja na jamii ya Watanzania kutokubali kuwa ajali za barabarani ni tatizo.

“Mfano wa nchi ya Japan, mara nyingi ajali zinazotokea katika taifa hilo la watu wengi ni kidogo sana ukilinganisha na nchi zetu,” anasema.

Ngowi anasema, chanzo kingine ni pamoja na sheria ya usalama barabarani kifungu cha kutoa adhabu ya kosa la ajali, hususan ajali ya kusababisha majeraha na kupoteza uhai.

Kifungu hicho, anasema, kimekuwa ni chanzo kikubwa cha ajali kwa sababu ya kujirudia rudia, hivyo ni vema kukiboresha au kukibadilisha.

”Pia suala la motisha, makubaliano kati ya dereva na mmiliki wakati mwingine motisha haionekani kwa uwazi na inafanya wakati mwingine dereva kuwa na mawazo, hivyo tusipoangalia vizuri motisha inakuwa sehemu ya chanzo cha ajali,” anasema.

Anaongeza: “Sababu nyingine ni madereva kuacha taaluma yake ya udereva aliyosomea na kufuata utashi wake mwenyewe ambapo dereva anaendesha gari kwa kadiri anavyojisikia. Kuna haja ya kufanyia utafiti vyanzo hivi vine.” 

Abdallah Lungo, Mwenyekiti wa Kamati ya Latra CC Mkoa wa Tanga, anasema ajali za barabarani zinachagizwa na madereva kuendesha vyombo vya usafiri kwa umbali mrefu bila kupumzika.

Akitoa mfano, akasema dereva anatoka Mbeya hadi Tanga anaendesha peke yake hana hata mpokezano wowote, hii inachangia kupoteza umakini na kusababisha ajali.

Anasema, katika baadhi ya maeneo ya matukio ya ajali, uchunguzi unabaini kuwa ndiyo maeneo hatari ambapo dereva anakuwa anasingizia na amechoka zaidi.

“Tuendelee kuhamasisha jamii kuelewa haki na wajibu wao wakiwa safarini ili kupunguza matukio ya ajali, ajali za barabarani zinazuilika endapo ushirikiano utakuwepo kati ya watumiaji wa barabara, wananchi na serikali,” anasema.

Naye Mkuu wa Elimu ya Usalama Barabarani wa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani, ACP Michael Deleli, anasema ajali nyingi za barabarani hasa za masafa marefu mara nyingi hutokea wakati dereva anapokaribia kumaliza safari yake.

Anasema ajali hizo zinatokea kwa sababu ya uchovu au uzembe wa kufikiria vitu vingine.

“Kwa wastani hayo makosa ya dereva yanajitokeza kutokana na uchovu wa safari lakini bado anajikaza kuendesha gari wakati anakuwa amechoka.”

Aidha, Daktari Anzibert Rugakingira kutoka Wizara ya Afya, anasema Wizara ina mpango wa kudhibiti magonjwa yasiyoambukizwa, ikiwemo afya ya akili na ajali.

”Ajali kwa nchi yetu zinaongezeka kwa kiasi kikubwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya utafiti takriban miaka 10 na kuonyesha Tanzania imekuwa nafasi ya 9 hadi ya 10 duniani kwa vifo na majeruhi wa ajali kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2020. 

”Takwimu zinatuonyesha kwamba kuna vifo zaidi ya 32,800, hii inamaanisha kwa kila siku kwa miaka 10 iliyopita kuna watu nane hadi tisa wanafariki kutokana na ajali Tanzania,” anasema.

Anasema, kwa sasa wizara imekuja na mpango na mkakati ambapo inashirikiana na wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya kama Kitengo cha Mifupa (Moi).

Jambo kubwa wanalolifanya ni kuelimisha jamii kwa kuwa wameona sababu zinajulikana zinazosababisha ajali kila mara kama mwendokaesi, matumizi ya vilevi, matumizi mabaya ya barabara pamoja na miundombinu.