November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwepo wa Boeing 767-300F na lengo la Rais Samia kukuza usafirishaji mizigo kupitia sekta ya anga

Na Frida Jahson,TimesMajiraOnline,Dar

NCHI yoyote duniani ambayo imedhamiria kujenga uchumi imara, lazima iwe na miundombinu thabiti inayorahisha mazingira ya ufanyaji biashara.

Hiyo ni kwa sababu hakuna nchi ambayo inaweza kuendelea kiuchumi kwa kutegemea soko la ndani la mauzo ya bidhaa zinazozalishwa na wakulima wake au viwanda.

Mauzo ya bidhaa nje ya nchi ndiyo yanawezesha Taifa kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Nchi kama haina miundombinu yake ya kusafirisha nje bidhaa, inakuwa tegemezi na moja ya kilio cha muda mrefu cha wafanyabiashara kutumia gharama kubwa kusafirisha bidhaa nchi ya nchi.

Miongoni mwa miundombinu rahisi za usafirishaji bidhaa katika masoko ya nje ni ndege za mizigo ambazo zinarahisha gharama za usafirishaji mizigo zikitumia muda mfupi na nchi inapokuwa na ndege zake, gharama zinakuwa ndogo.

Ushahidi wa Tanzania kuwa na mahitaji makubwa ya ndege za mizigo ni kilio cha muda mrefu cha wafanyabiashara wanaotumia viwanja mbalimbali nchini kusafirisha mizigo yao.

Miogoni mwa wafanyabiashara hao ni wale wanaotumia Uwanja wa Ndege wa Mbeya. Kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine wanaotumia viwaja vya ndege kusafirisha mizigo yao, huko nyuma iliwabidi wasubiri zaidi ili kupata huduma hiyo kutokana na kutokuwepo kampuni iliyojitokeza kutoa huduma ya ndege za mizigo kupitia viwaja vingi nchini.

Miongoni mwa viwanja hivyo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) unaotegemewa zaidi na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Iringa, Mbeya na Njombe na Songwe.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya Meneja wa Uwanja SIA, uwanja huo unahudumia wastani wa tani 55,000 kwa mwezi takriban mara 10 ya kiwango cha uwanja wa zamani uliokuwapo katikati ya jiji.

Hata wakati kukiwa na ndege za abiria pekee ambazo bado hazikidhi mahitaji hasa ikizingatiwa Mbeya ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa kuwa na viwanda vingi nchini ambavyo baadhi ya bidhaa zinazozalishwa husafirishwa kwenda mikoa mingine na hata nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), bado changamoto ilikuwa ni nchi yetu kutokuwa na ndege za mizigo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Rapha Group, inayomiliki kiwanda cha kusindika mazao ya nafaka Jijini Mbeya, Raphael Ndelwa, aliwahi kunukuliwa huko nyuma akisema pamoja na SIA kufungua masoko ya ndani na nje, bado kutokuwepo kwa ndege za mizigo kilikuwa ni kikwazo kwa kuwa ndoto zao hazikuwezi kutimizwa.

Mwonekano wa ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F

Ndelwa alinukuliwa akisema kwa mwezi husafirisha nafaka za aina mbalimbali kwenda nje ya mkoa ukiwemo mchele kati ya tani 500 hadi 1,000, maharage tani 30 hadi 25, na wakati mwingine oda huwa inaongezeka zaidi.

Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuanza kununua ndege za mizigo akianza na ndege aina ya Boeing 767-300F iliyowasili Juni, 2023 ni kielelezo cha usikivu wa kilio cha wafanyabiashara na anaelewa umuhimu wa ndege za mizigo.

Hii inadhihirishwa na kauli ya Rais Samia aliyoitoa kuhusiana na uamuzi wake wa ununuzi wa ndege ya mizigo akisema;

“Serikali imeamua kununua Ndege ya kusafirisha mizigo kwa sababu nchi yetu ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa matunda, mbogamboga na maua.”

Akithibitisha hilo Rais Samia alisisitiza; “Mwaka 2019, Tanzania iliuza nje mazao yenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 700 na inatarajia hadi kufikia mwaka 2025 kuingiza Dola za Marekani bilioni 2.”

Matamanio ya Rais Samia ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 Tanzania iweze kuingiza dola milioni 2.

Dhamira hiyo ya Rais Samia inawezekana kwani tayari ndege ya mizigo aliyonunua ikisimamiwa na Kampuni ya Ndege Air Tanzania (ATCL) imeanza safari zake.

Wafanyakazi wakipakia mizigo kwenye ndege mpya ya mizigo iliyonunuliwa na Serikali aina ya Boeing 767-300F ikiwa ni maandalizi ya kuanza safari.

Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ATCL, Patrick Ndekena, wakati wa safari yake ya kwanza ya ndege hiyo katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salam, alisema;

“Leo tunafuraha kubwa kwa kuanza rasmi safari zetu za ratiba kwa ndege yetu hii mpya ya mizigo Boeing 767-300F yenye uwezo wa kusafiri masafa marefu na uzito mkubwa yaani tani 54 kwa mara moja, kwa Dubai peke yake tutakuwa na safari mbili kwa wiki, Jumatatu na Ijumaa.”

Kuhusu uwezo wa ndege hiyo, alisema Boeing 767-300F ni ndege ya kisasa yenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 850 kwa saa na kukaa angani kwa zaidi ya masaa 10 bila kutua.

Kuhusu wataalamu wa ndege hiyo alisema ATCL ina marubani wakitanzania sita waliobobea kwenye ndege hii. Wataalam wengine wabobezi ni pamoja na wahandisi wa ndege ambao pia ni Watanzania.

Ndekana amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuiwezesha ATCL kujiendesha kibiashara.

Naye wakala wa usafirishaji mizigo, George Magoti alisema uwepo wa ndege hii ni mkombozi kwa wafanyabiashara nchini, kwani itawasaidia kupunguza gharama za usafirishaji.

Magoti alifafanua kwamba kutokana na ukubwa wa mizigo hii, isingewezekana kusafirishwa kwa ndege ya abiria, hivyo wangelezimika kukodi ndege ya mizigo kutoka nje ya Tanzania ili kuweza kupakia mizigo mikubwa ya aina hii.

“Tunashukuru ATCL kukubali kufanyabiashara nasi ya mizigo la sivyo tungelazimika kutafuta ndege kutoka nchi zingine ambapo ingeongeza gharama, kuchelewesha muda kusubiri ndege ifike na usumbufu wa vibali vya hiyo ndege ya nje,” alisema Magoti.

Alifafanua kuwa mzigo uliopakiwa na Air Tanzania utapelekwa hadi Dubai na kutoka hapo utasafirishwa kwenda Marekani kwa urahisi na uharaka kuliko wangetumia usafiri mwingine.

Alisema mpango wa ununuzi wa ndege ya mizigo umelenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka na kuingia Tanzania na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa nchini.

Mmoja wa wafanyabiashara (jina tunalo) anasema ndege hiyo imeanza kupunguzia wafanyabiashara gharama za usafirishaji, hasa wa bidhaa za maua, mbogamboga, nyama na samaki.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema ndege hiypo imerahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi.

“Ujio wa ndege hii umeleta unafuu kwa wafanyabiashara, hasa wa mbogamboga, maua, nyama, samaki na madini na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje na Serikali pamoja na wafanyabiashara, hususani wa dawa,” alisema.

Wakizungumzia ujio wa ndege hiyo, wadau wa sekta hizo wameipongeza Serikali kwa kununua ndege hiyo na kwamba itawasaidia kupata uhakika wa kusafirisha bidhaa zao kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda (Taha), Jacqueline Mkindi alisema kama ndege hiyo itakwenda kwenye masoko ya Ulaya wanakopeleka bidhaa za maua na mbogamboga, itakuwa ni nafuu kwa mazao yao yanayotegemea usafiri huo.

“Masoko ya horticulture (maua, mbogamboga na matunda) yanayotumia usafiri wa ndege yako Ulaya, kama ndege itakwenda Ulaya itakuwa na faida kubwa sana kwetu,” alisema Mkindi.

Aidha ununuzi wa ndege ya mizigo utaimarisha usafirishaji wa minofu ya samaki moja kwa moja kwenda nje ya nchi kutokea uwanja wa ndege wa Mwanza.

Rais Samia akiwa kwenye chumba cha marubani cha ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F mara baada ya kuwasili nchini. Anayekutazama ni rubani mwanamke Mtanzania aliyeleta ndege hiyo hapa nchini

Akizungumza hivi karibuni kwenye mkutano wa kupokea mikakati ya pamoja kuondoa vikwazo na kufanikisha biashara ya usafirishaji minofu ya samaki kwenda nje ya nchi hususani mataifa ya Ulaya ambako kumekuwa na soko la uhakika, mmoja wa wafanyabiashara, Patric John alisema;

“Ununuzi wa ndege hizo utarahisisha biashara ya samaki na nchi zingine, hivyo taifa litapata fedha nyingi za kigeni.”