Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
UWEKEZAJI wa ujenzi wa vivuko uliofanywa na Serikali umetajwa kuwa kichocheo muhimu cha kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na usalama wa taifa, hususani maeneo yenye miundombinu ya maji.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Mwanza na Mkufunzi Mwandamizi Elekezi, Jeshi la Nchi Kavu kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), Brigedia Jenerali. Method Matunda, mara baada ya wanachuo wa chuo hicho, kutembelea miradi mitano ya ujenzi wa vivuko inayotekelezwa katika karakana ya Songoro Marine.

Brigedia Jenerali Matunda amesema, vivuko ni nyenzo muhimu si tu katika kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na mali, bali pia ni mkakati wa ulinzi wa taifa katika maeneo yanayotenganishwa na maji.
Amesema ziara hiyo ya mafunzo mkoani Mwanza ilitanguliwa na Mkoa wa Geita, ambapo asubuhi walitembelea uwanja wa ndege wa Mwanza kabla ya kufika Songoro Marine, kampuni ambayo imejenga zaidi ya vivuko 30 kwa ajili ya Serikali.
“Songoro Marine ni mdau mkubwa katika ujenzi wa vivuko nchini. Vivuko hivi vina mchango katika kuunganisha maeneo ya nchi kavu na yale ya maji, jambo ambalo ni muhimu katika usalama na maendeleo ya taifa,” amesema.
Amesema katika masuala ya ulinzi, uwezo wa kusafirisha haraka vyombo vya ulinzi katika maeneo yenye maji ni jambo lisiloweza kuepukika, hivyo uwepo wa vivuko vya uhakika unaimarisha utayari wa kiulinzi.
“Suala la ulinzi wa nchi sihitaji kueleza kwa mtu yeyote.Naamini popote tunapohitaji kupeleka vyombo vya ulinzi kusimamia usalama katika maeneo yenye maji yanayounganishwa na barabara, vivuko ni lazima vinavihitajika,”amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Songoro Marine, Mohamed Salehe, ameishukuru Serikali kuendelea kuwaamini wakandarasi wa ndani na kuwapa fursa ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati,jambo ambalo linawapa motisha ya kuongeza ubora na ufanisi katika kazi zao.
“Tumejawa na faraja kubwa kutembelewa na Chuo cha Ulinzi cha Taifa. Tunajisikia fahari kuwa sehemu ya maendeleo na ulinzi wa nchi yetu,”amesema.
Maaofisa hao wanafunzi wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa wanatoka Tanzania pamoja na nchi za Rwanda, Burundi, Zimbabwe, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Misri na Ethiopia, wako katika ziara ya siku sita mkoani Mwanza, itakayohitimishwa Januari 24, 2026.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi