November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

UWEKEZAJI uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya umeendelea kuipaisha Tanzania ambapo sasa madakati bingwa wanne wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI wako nchini Zambia kufanya upasuaji wa moyo.

Timu hiyo ya madakari hao itashirikiana na wenzao wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia na watafanyakazi upasuaji wa moyo kwa muda wa wiki moja .

Mkuu wa ujumbe huo, Dkt. Viviane Mlawi wa (JKCI), ambaye ni daktari bingwa wa moyo kwa watoto, alisema ujumbe huo pia umeambatana na mtaalam mbobezi wa chumba cha upasuaji na mtaalamu wa usingizi katika upasuaji Moyo.

Alisema wameambatana pia na mbobezi katika kuhudumia wagonjwa wa nje wanaokuja kupata matibabu Tanzania, Dk. Maiyer Msengi na wauguzi wawili ambao ni wabobezi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Dkt. Mlawi alisema malengo makubwa ya safari hiyo ni matano ambayo ni kufanya upasuaji wa moyo kwa wahitaji ambao ni wengi nchini Zambia na kuwajengea uwezo madaktari wa Zambia mbinu za upasuaji ambazo bado hawajawa nazo na kubadilishana ujuzi.

Alitaja lengo lingine kuwa ni kukagua kwa pamoja na kubainisha maeneo ambayo Tanzania inaweza kushirikia na Zambia katika kuwasaidia wazambia matibabu ya kibingwa kwa wepesi na gharama nafuu.

Dk. Mlawi alisema madaktari hao watakagua na kubainisha vifaa tiba ambavyo vipo na vile ambavyo havipo ili kuweka mikakati ya jinsi gani wanaweza kushirikiana kuvipata ili kuboresha huduma zao.

Alitaja lengo lingine kuwa ni kuona maeneo mbalimbali ya ushirikiano katika tafiti, teknolojia na mambo ya msingi ambayo Tanzania iko mbele sana katika eneo hilo kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Naye Dk. Maiyer ambaye ni mtaalam wa usimamizi wa wagonjwa kutoka nje ya nchi, alisema yapo mambo mengi ambayo JKCI na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia wanaweza kuyafanya kwa kushirikiana kwaajili ya maendeleo ya nchi hizo mbili.

Alitaja masuala hayo kuwa ni kuhakikisha wanarahisisha utoaji wa vibali vya kuingia kwenye nchi hizo (visa), malazi kwa wanaotembelea nchi hizo na usajili wa mawasiliano ya namba za simu na vibali vya kwenda kupata matibabu.

Alisema kwa upande wa Tanzania watahakikisha kunakuwa na uhakika wa miadi ya kukutana na madaktari bingwa na kupata huduma kwa wakati ili kupunguza gharama za kuishi nchini kwa muda mrefu .

Alisema watahakikisha kunakuwa na huduma bora wakati na baada ya upasuaji wa wagonjwa wa moyo na kufanya JKCI iendelee kuwa kimbilio kwa mataifa mengi ya Afrika na kwingineko.

Alisema jambo lingine la msingi ambalo watahakikisha linazingatiwa ipasavyo ni uhakika wa gharama sahihi za vipimo na matibabu na usalama wa mgonjwa kwa kulinda haki zake zote akiwa anapata matibabu.

Alisema kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili katika utoaji wa taarifa ubalozini hasa kwa kuzingatia kuwa kuna mahitaji makubwa ya watu kuja nchini kupata matibabu ya moyo.

Msemaji wa Hospitali ya Moyo ya Taifa ya Zambia, Dk. Chabwela Shumba alisema wamekutana na madaktari wa Tanzania na baada ya kufanya uchambuzi wa uwekezaji ambao serikali imefanya kwa JKCI wameona kwamba watanufaika kwa kiwango kikubwa kama watashirikiana na Tanzania.

“Tumeshangaa sana kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa katika vifaa vya kisasa kama MRI, CT SCAN, rasilimali watu, teknolojia na kiwango kikubwa cha wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo kwa mafanikio makubwa,” alisema Shumba.

Alisema wamebaini kuwa JKCI inateklojia ile ile inayotumiwa na mataifa yaliyoendelea hivyo hakuna haja ya kuwapeleka wagonjwa wao kwenye nchi hizo kwani wanaweza kupata huduma kama hizo taasisi ya JKCI.