December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akipokea maelezo kuhusu ufugaji wa ngamia katika shamba la Highland Estate kutoka kwa Mkurugenzi wa shamba hilo Pirmohamed Mulla alipotembelea moja ya uwekezaji wa kampuni hiyo ya ufugaji wa ng’ombe na ngamaia katika shamba hilo lililopo Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ikiwa ni ziara yake ya kutembelea maeneo ya uwekezaji juzi. (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Uwekezaji tunaoutaka ni ule wa kuwajibika katika jamii – Waziri Kairuki

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Nchini Angellah Kairuki amewataka wawekezaji wote nchini kujihusisha na jamii zinazowazunguka kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuleta tija ya uwekezaji wao.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akipokea maelezo kuhusu uvunaji wa kisasa wa mpunga kutumia mashine aina ya combine harvester zenye uwezo wa kuvuna tani 2.5 katika shamba la Estate kutoka kwa Mkurugenzi wa shamba hilo Bw. Pirmohamed Mulla alipotembelea shamba hilo lililopo Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Waziri Kairuki amesema hayo katika ziara ya kutembelea maeneo ya uwekezaji ili kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika uwekezaji wao.

Waziri Kairuki alitembelea kampuni inayojishughulisha na kilimo cha mpunga ya Highland Estate iliyopo katika Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya mwishoni mwa wiki.

Akiwa katika ziara hiyo, Kairuki amewataka wawekezaji wote nchini kuwajibika katika jamii zinazowazunguka ili kuendelea kuwa na mchango chanya kwa jamii kwani kufanya hivyo kutaboresha uhusiano mzuri kati yao na jamii inayowazunguka.

“Tunawashuru kwa namna mnavyowajibika katika jamii, huo ndiyo uwekezaji tunaoutaka, pamoja na nyie kupata faida ni vyema kuwajibika katika jamii inayowazunguka, jamii ambayo uwekezaji wako upo, tumeelezwa maeneo mengi ambayo mmetoa mchango wenu zikiwepo shule, kuchangia huduma za afya, mnavyojenga mabanio mapya, ujenzi wa kituo cha polisi na mengine mengi.” amesema Kairuki

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki (mwenye barakoa) akiangalia ng’ombe aina ya boran waliopo katika shamba la kampuni ya highland Estate. Anayetoa maelezo ya ng’ombe hao ni Mkurugenzi wa shamba hilo Pirmohamed Mulla (mwenye kofia), waziri alitembelea shamba hilo lililopo Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ikiwa ni ziara yake ya kutembelea maeneo ya uwekezaji.

Aidha ameeleza mikakati ya serikali katika kuhakikisha inaboresha mazingira ya wawekezaji na wafanyabiashara nchini hivyo ni vyema kuzitambua na kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo na kuzikumbuka jamii zetu.

“Serikali kwa sasa inaendelea kuboresha mazingira bora ya biashara na uwekezaji, na kwa upande wa kilimo hii ni sekta ambayo tunaipa kipaumbele sana tukitambua kuwa ni sekta inayoajiri watu wengi lakini ina mnyororo mrefu wa thamani na wanufaika ni wengi” amesema Waziri Kairuki

Upande wake Meneja Msaidizi wa shamba hilo Sadiki Wigira amesema kuwa, sambamba na uzalishaji wa mpunga, kampuni inajishughulisha na kilimo cha matunda, mbogamboga, zao la korosho, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa pamoja na ng’ombe wa nyama na vilevile wanamatarajio ya kuanzisha kiwanda cha kusindika nyama na maziwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Aswege Kaminyoge amemshuruku Waziri Kairuki kwa kufanya ziara katika wilaya hiyo na kutembelea kampuni ya Highland Estate kwani kampuni hiyo pamoja na kampuni zingine zilizopo hapa zimekuwa zikitoa ushirikiano mzuri kwa serikali kwa kulipa kodi zote za halmashauri bila usumbufu na amewataka kuendelea kushirikiana ili kuboresha uchumi wa nchi yetu.

Waziri Kairuki ameipongeza kampuni ya Highland Estate kwa uwekezaji walioufanya katikka eneo la Mbarali kwani uwekezaji huo umetoa ajira kwa wakulima zaidi ya 4,000 wa makundi mbalimbali pamoja na ajira za kudumu zaidi ya 310.

Vilevile zaidi ya wakulima 20,000 wamenufaika katika huduma mbalimbali zikiwemo huduma za ugani, mafunzo, vitendea kazi, pembejeo za kilimo, mbinu bora za kilimo pamoja na fursa za ardhi yao kwa wakulima wadogowadogo ambao hawamiliki ardhi.

Afisa Mipango Wilaya ya Mbarali Emmanuel Kishimbo akisoma taarifa ya masuala ya uwekezaji katika Wilaya hiyo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki alipotembelea katika Wilaya hiyo kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji katika sekta ya kilimo wilayani humo mkoani Mbeya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Highland Estate Fahad Haroon wakati wa ziara yake katika shamba la mpunga linalomilikiwa na kampuni hiyo katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akizungumza na wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipotembelea katika Ofisi za chama hicho Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya, Hashmu Mwaliyawa na kulia ni Katibu Siasa na Wenezi, Kassim Kondo.