Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Dar
MIKAKATI na dhamira aliyonayo Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha Tanzania inakuwa ghala la chakula barani Afrika.
Rais Samia anasema Serikali imeishaanza kuwekeza kibajeti na kimkakati katika maeneo ya msingi kwenye kilimo, hivyo anataka Watanzania watumie vyema fursa zilizopo kuionesha dunia nia ya nchi ya kuwa ghala la chakula Barani Afrika.
Pamoja na kuwekeza kibajiti na kimkakati, Rais Samia ameenda mbali zaidi kwa kuunda Baraza la kumshauri kuhusiana na masuala ya kilimo linaloongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda.
Ili kufikia dhamira hiyo ya Rais Samia, Wizara ya Kilimo kupitia Benki ya Mandeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati za kuwezesha wakulima ili Tanzania iweze ghala la chakula Afrika.
Kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wizara ya Kilimo pamoja na TADB, inaonekana wazi mikakati na dhamira hiyo ya Rais Samia ya kuwezesha Tanzania kuwa ghala la chakula Afrika inawezena.
Hiyo inathibitishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURA), Sadala Chacha, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea chama hicho ili kujionea uzalishaji wa mpunga katika Bonde la Mtu Ruvu.
Kwa kudhihirisha hilo, Sadala anasema; “Dhamira ya Rais Samia ya Tanzania kuwa ghala la chakula barani Afrika inawezekana, kwani kupitia mikopo inayotolewa TADB, tumezidi kuongeza uzalishaji kwenye shamba la Mpunga lililopo Ruvu ambalo chama hiki kimekabidhiwa na Serikali.”
Chama hicho kilirithi shamba hilo kutoka National Agricultural Corporation (NAFCO) kufuatia uamuzi wa Serikali wa ubinafsishaji mashirika ya umma, ambapo shamba hilo lilikabidhiwa kwa wakulima wadogo wadogo wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Sadala anasema CHAURA ilianzishwa mwaka 2002 ikianza na wanachama 160, lakini hadi sasa wamefikia 900, ambao wanaendesha kilimo kwenye shamba hilo, wakiwa miongoni mwa wakulima wanaotarajiwa kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula Afrika.
Kwa mujibu wa Sadala kabla ya kukabidhiwa wao shamba hilo, lilikuwa ni pori, ndiyo maana Serikali iliamua kuwapa wakulima wadogo wadogo ambao baadaye waliamua kuanzisha ushirika.
Shamba hilo lina ukubwa wa hekta 3,200, lakini eneo lenye miundombinu ya umwagiliaji ni hekta 720 sawa na ekari 1,800. Wakati wanakabidhiwa shamba hilo, Sadala anasema NAFCO walikuwa wanalima ekari 71 na walikuwa wanavuna tani 0.9 kwa hekta.
Anaeleza kwamba baada ya shamba hilo kukabidhi kwenye Ushirika, walianza kuvuna tani 3 kwa hekta, lakini kwa sasa wanavuna tani 9.5 hadi 9.7 kwa hekta baada ya kuanza kupata mkopo kutoka TADB.
Anafafanua kuwa walianza kufanyakazi na TADB kwa kupatiwa mkopo mwaka 2018, hivyo kuongeza kiwango cha eneo kilimo, wakiwa na uwezo wa kulima hekta 480 hadi 500.
“Lakini sasa hivi tumefikia kulima hekta 720 sawa na ekari 1,800, tumefikia kulima hekta hizi kutokana na ushirikiano kati ya CHAURU na TADB kupitia mikopo,” Anasema Chacha.
Kwa mujibu wa Chacha, hadi sasa CHAURA imepatiwa mkopo kwa nyakati tofauti kutoka TADB unaofikia sh. 1,333,000,000 na kwamba hicho ni kielelezo, kinachodhihirisha Serikali imedhamiria kuwawezesha wakulima.
Anasema mkopo huo umeiwezesha CHAURA kuongeza kiwango cha uzalishaji. Anapongeza Serikali kwa kuanzisha TADB, kwani utaratibu wake wa utoaji mkopo hauna masharti magumu, wala hauhitaji dhamana kama ilivyo kwa taasisi nyingine za fedha.
Anatoa mfano kuwa kabla ya kuanza kupata mkopo kutoka TADB, mwaka 2009 waliomba mkopo kutoka taasisi moja ya fedha na baada ya mazungumzo, waliambiwa hawawezi kukopeshwa kwa sababu hawana dhamana na shamba hilo ni mali ya Serikali.
Kwa msingi huo, Chacha anasema ilikuwa vigumu kuongeza uzalishaji, kwani wakulima walikuwa wanakopa fedha kutoka kwa wachuuzi kwa ajili ya kununulia mbolea na pembejeo.
“Hivyo hata walivyokuwa wakivuna, walikuwa hawasubiri bei iwe nzuri kwenye soko ndipo wauze, kwani walikubaliana na wachuuzi kilo ya mpunga wauziwe kwa sh. 400, hivyo hata kwenye soko mpunga ungeuzwa sh. 1,000 kwa kilo, mkulima alilazimika kumuuzia mchuuzi kwa sh. 400, hivyo hawakuwa na uwezo wa kukataa,”anasema Chacha.
Chacha, anafafanua kwamba baada ya kuanza kupata mkopo kutoka TADB, wachuuzi hawana nafasi tena na wao kama ushirika, ndiyo wanaowakopesha na ndiyo maana wameanza kuwa na maendeleo makubwa.
“Kupitia mikopo hiyo, kwa sasa kila mkulima wanahakikisha anatumia mifuko sita ya mbolea kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari moja,”anasema Chacha.
Tunawakopesha pembejeo na wanafanya marejesho baada ya mavuno, hatua ambayo imeongeza mavuno kutoka tani nne kwa ekari hadi sita hadi saba kwa mwaka jana.”
Kwa mujibu wa Chacha, mkopo wanaukopa benki kama chama na wao kukopesha mkulima mmoja mmoja, hali ambayo imechangia uzalishaji kuzidi kuongezeka.
Aidha, anasema wameweza kulima shamba lote baada ya chama kuanza kuwakopesha zana za kilimo na pembejeo.
“Mikopo ya pembejeo tunakopeshwa mikopo ya muda mrefu na muda mfupi, ambapo mkopo wa trekta tulishamaliza kuulipa. Lakini kila mwaka tumekuwa tukikopa mkopo kwa ajili ya pembejeo,”anasema.
Kwa upande wa miundombinu ya kilimo kwenye shamba hilo, Chacha anasema wakati wanarithi shamba hilo, miundombinu yake ilikuwa imechakaa kwani ilijengwa tangu 1965.
Lakini kutokana na mkopo waliopata kutoa TADB, wameweza kukarabati miundombunu ya shamba ikiwemo ya umwagiliaji ndiyo maana mavuno yameongezeka.
Anaeleza kwamba kwa sasa ekari moja inazalisha magunia 25 hadi 30 ya mpunga, lakini kabla ya hapo mavuno yalikuwa kati ya magunia nane hadi 10 kwa ekari.
“Awali upotevu wa maji ulikuwa asilimia 80, lakini tumeupunguza kwa kiasi kikubwa na hii ni matokeo ya mkopo kutoka TADB, lakini pia fedha ambazo chama kinapata kwa kuwalimia wakulima, nazo tunaziwekeza kwenye ukarabati wa miundombinu,” anasema Chacha.
Anasema mkakati wao ni kubadilisha Scheme hiyo ili iwe ya mfano kwa Tanzania nzima.
Anasema kwa hatua ambayo amefikia, TADB, ilikuwa wanatambaa, lakini sasa hivi wameanza kutembea na kukimbia, kwani tayari wamenunua, kwani mbali na kutumia mkopo huo kununua zana za kilimo, mbolea pamoja na pembejeo, wameweza kununua pampu mbili kwa ajili ya umwagiliaji kutoka China, wamejenga mfereji wenye urefu wa mita 700 na wanaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mingine.
Anasema malengo yao kama chama ni ifikapo mwaka 2028 hadi 2030 CHAURA kiwe chama cha mfano.
Kuhusu mpato, anasema utaratibu waliojiwekea chama kimekuwa kikimlimia, kummwagilia shamba lake msimu mzima na baada ya kuvuna, kila mwanachama anachangia kwenye chamba mpunga kilo 80, sawa na kilo 160 kutoka kwenye ekari mbili ambazo kila mkulima analimiwa.
Anasema chama kina mashine zake za kukoboa, hivyo wanakomboa na kuuza mchele na mapato yanakuwa ya chama kwa ajili ya kuendelea kuboresha miundombinu ya shamba. Aidha, anasema kuna michango mingine ambayo wamekubaliana kama chama.
Akieleza mkopo ambayo wamekopa TADB, Chacha anasema mkopo wa kwanza walikopo 2018-2019 kiasi cha sh. milioni 450, mwaka wa pili walikopeshwa sh. milioni 140.
Aidha, anasema walikopeshwa tena sh. milioni 480 kwa ajili ya mkopo wa pembejeo.
Anasema msimu ambao umeisha walikopeshwa sh. milioni 695 kwa ajili ya pembejeo, ambapo waamegiza mbolea kwa ajili ya wanachama wao kutokana nje.
Kwa sasa anasema wameanza mchakato wa kuomba mkopo mwingine kutoka TADB wa sh. milioni 840.
Chacha, anasema ndani ya shamba hilo, kuna eneo lenye ukubwa wa hekta 1,500 sawa na ekari 3,000 bado halijaendelezwa, hivyo wao na TADB bado wana safari ndefu.
Kwa hiyo anasema wana mpango wa kuchukua mkopo ili kuongeza mifumo ya umwagiliaji ili angalau kila mkulima alime ekari tano badala ya mbili za sasa.
Aidha, anasema wana matarajio ya kuongeza idadi ya wanachama, hivyo ni lazima eneo la kilimo liongezeke.
Mmoja wa wakulima, Anna John, anapongeza Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia, kwa kuendelea kuhakikisha Benki ya TADB inazidi kuwakopesha wakulima ili waweze kuzalisha zaidi na hatimaye kufikia malengo ya Serikali.
More Stories
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Maono ya Samia ujenzi shule maalum za wasichana kuzalisha wanasayansi
Wasaidizi wa Rais Dkt. Samia wanavyokuna vichwakuhakikisha Tanzaniaa inufaika na ahadi za FOCAC