Na Agnes Alcardo, Timesmajira online, Dar es Salaam
UMOJA wa watu wenye ulemavu Waendesha Bajaji jijini Dar-es-Salaam (UWAWABADA), umeiomba Serikali kurudisha utaratibu wa awali wa kuzuia pikipiki za matairi matatu (Bajaji), zinazoendeshwa na watu wasiyo na ulemavu kuingia katikati ya mjini pamoja na kuwatofautishia maegesho.
Ombi hilo, limetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Watu wenye Ulemavu Tanzania (CHAWATA), Hamad Komboza, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliyekuwa mgeni rasmi, kwenye mkutano mkuu wa umoja huo uliokuwa na lengo la kusikiliza changamoto zao.
Komboza amesema, kati ya changamoto wanazokutana nazo madereva bajaji wenye ulemavu ni kuchanganyika na wasiyo na ulemavu wanapoingia katikati ya mji, hali inayowasababisha kukosa abiria kwani wao hawawezi kushindana na wazima, huku changamoto nyingine ikielezwa kuwa ni maegesho ya bajaji ya pamoja.
” Tunaomba Serikali iliangalie hili suala kwa kuturudishia utaratibu ambao ulikuwa awali wa kutoruhusu waendesha bajaji wasiyo na ulemavu wa viungo kuingia mjini, kwani hali hiyo inampa wakati mgumu mtu mwenye ulemavu kupambana na mtu asiye na ulemavu katika kugombania kupakiza abiria,”amesema Komboza.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, ameutaka umoja huo kuwa na utulivu na kuwahakikishia kuwa, Serikali itazitatua changamoto zao ikiwa pamoja na kuwepo kwa utaratibu wa vyombo vyote vitakavyoingia katikati ya jiji kuwekewa alama na namba za utambuzi.
Lakini pia, amesema Serikali bado inaendelea kushughulikia changamoto za maeneo ya maegesho, muingiliano na watu wasiyo na ulemavu pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa kundi hilo maalum.
Mpogolo amesema uamuzi huo unatokana na kikao cha kamati ya usalama barabarani, baada ya kukubaliana juu ya jambo hilo, huku akidai kuwa bado suala hilo linasubiri baraka za vikao vingine na kisha kuundiwa sheria ndogo ili liweze kufanyika.
” Tunaweka alama na namba ili yeyote atakayeingia katikati ya mji mtajua huyu si mwenzenu,hivyo niwaombe mnapokuwa mnajadili na kuazimia wekeni na utaratibu wa nini kifanyike kwa atakayekwenda kinyume na maazimio yenu,”amesema Mpogolo.
Pia, ametoa onyo kwa wale watakaobainika kuchukua bajaji za wenye ulemavu na kuziendesha katika maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya walemavu na huku wao wakiwa si walemavu kuwa sheria itachukua mkondo wake, huku akiwasisitizia kuwa Serikali inaowajibu wa kuwalinda.
Huku akitumia fursa hiyo kuwataka kufuata sheria za usalama barabarani kwa kudai kuwa wapo wanaopita taa nyekundu zikiwa zimewaka huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â