December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uvuvi: Masoko ya nje kupaisha uchumi wa nchi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Sekta Yenye Matumaini

Sekta ya Uvuvi ni miongoni mwa sekta muhimu za uchumi nchini inayochangia katika Pato la Taifa na kuondoa umaskini.

Sekta hii inajumuisha shughuli zote za uvuvi wa asili na ukuzaji wa viumbe maji kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisasa.

Kwa mwaka 2022, sekta ya uvuvi ilikuwa kwa asilimia 2.5 na ilichangia silimia 1.8 ya pato la taifa.

Takriban Watanzania milioni 4.5 wamepata ajira kupitia sekta ya uvuvi katika mnyororo mzima wa sekta hiyo huku ajira za moja kwa moja za wavuvi zikiwa 195,000 na wakuza viumbe vya majini 31,998.

Tanzania: Utajiri wa baharini
Tanzania kuna bahari, mito, maziwa ambayo yanaweza kutumika vizuri kwenye uvunaji wa viumbe maji watakaoweza kusafirishwa na kuuzwa kwenye masoko ya nje ya nchi kupitia soko huria la nchi wanachama.

Kwa mwaka 2021/2022 meli 6 zilipatiwa vibali kwa ajili ya uvuvi mkubwa wa kibiashara ambapo meli 3 ni za nje ya nchi na 3 ni za wawekezaji wa ndani.

Bado kuna fursa kubwa kwa wawekezaji wa ndani kulichangamkia soko hili kubwa;
Vijana wengi wa Kitanzania wanaona kufanya biashara nje ya nchi ni jambo lisilowezekana.

Kwa kawaida ni ngumu kwa kijana aliyehitimu chuo na aliyepo mtaani kuzitazama fursa za nje ya nchi kwani wengi wanaamini ni kitu kigumu na kisichowezekana.

Hivyo inapelekea vijana wengi wajasiriamali wadogo hata wakubwa kuwekeza nguvu nyingi nchini pekee bila kuwa na mawazo ya kuvuka mipaka na kuanzisha viwanda, makapuni nje ya Tanzania.

Ukosefu wa elimu mahususi juu ya uwekezaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi ni kikwazo kwa vijana wengi wa Kitanzania hasa walihitimu vyuo vikuu.

Kwakuwa mfumo wa elimu unamtaka mwanafunzi ajue zaidi katika masomo ya darasani hii imefanya wanafunzi wengi wa vyuo kutojua mambo mengine ya kibiashara nje ya masomo.

Mfano mwanafunzi anayechukua masomo ya Kiswahili na historia, ni ngumu kujihusisha na masomo ya biashara, namna ya kuanzisha kampuni nje ya nchi, namna ya kusafirisha bidhaa bandarini na kadharika.

Hii inapelekea vijana kutojiingiza kwenye biashara zinazojumuisha Bara la Afrika.

Ahadi ya Eneo la Biashara Huria
Itakumbukwa mwaka 2021 serikali ya Tanzania iliridhia mkataba wa eneo huru la biashara bara la Afrika (AfCFTA) na hivyo kuwa nchi ya 41 kati ya nchi 55 za Kiafrika zilizoridhia mkataba huo utakaowezesha nchi wanachama kufanya biashara bila vikwazo vya ushuru wa forodha.

Hatua hii ni ya kupongezwa na kama ikiwekewa mikakati Madhubuti basi tatizo la ajira nchini litapungua kwa kiasi kikubwa:

Tanzania imebarikiwa maziwa, mito na bahari ya Hindi ambazo zote kwa Pamoja zinaweza kutumika kimkakati kutumia fursa za ACfTA kuzalisha bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu na kuzisafirisha katika nchi za Kiafrika ambazo hazina bahari.

Hii inaipa Tanzania fursa za kujiimarisha kwenye uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu zikiwemo aina kadhaa za samaki.

Kifuatacho ni Kipi?

Wizara ya Mifugo na Uvuvi haina budi kueneza elimu kwa wahitimu wa vyuo vikuu juu ya fursa zilizopo kwenye sekta hiyo, huku ikiweka mkakati wa kuwawezesha kwa teknolojia za kisasa ( visimba) na mabwawa kwa ajili ya uzalishaji mkubwa na wenye tija kuweza kushindana kwenye soko hilo Afrika.

Pia kulifanya somo la uvuvi kama sehemu ya masomo kwenye mitaala yetu itawezesha vijana wengi kutambua fursa nyingi zilizomo kwenye uchumi wa buluu.

Hii ina maana kuwa kama elimu ya uvuvi na bidhaa zitokanazo na bahari itatolewa kuanzia chini na vyuo vikuu basi vijana wanaohitimu vyuo vikuu watapata mwanga mkubwa wa nini cha kufanya kujiajiri kwenye uchumi wa buluu na usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buruu nje ya Tanzania Kwenda nchi zingine za Kiafrika.

Mabalozi wa Tanzania Uganda, Rwanda, Botswana hawana budi kuweka mikakati ya kutangaza utajiri wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu zilizopo nchini Tanzania.

Hapa kuna haja ya ubalozi kufanya ushirikiano wa kimkakati na wizara za biashara, sayansi na kilimo katika nchi husika ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa sahihi zinazohitajika katika nchi hizo.

Sambamba na hilo, kuna umuhimu wa ubalozi kuratibu ziara za kibiashara na uwekezaji kwa vijana wa Kitanzania wanaojihusisha na bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu ili wakajionee soko na uhitaji halisi wa bidhaa hizo katika nchi husika.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi itoe vibali vingi kwa wakati bila urasmu kwa vijana wa Kitanzania walio tayari kusafirisha bidhaa za zitokanazo na uchumi wa buluu Kwenda kwenye nchi husika.

Kama vibali hivi vitatolewa kwa wakati na kwa mashariti nafuu na rahisi basi vijana wengi watajitokeza kuchangamkia fursa hii itakoyopaisha pato lao na taifa kwa ujumla.

Michezo, Muziki ni miongoni mwa vitu vinavyowakutanisha vijana wengi, kama wasanii na wanamichezo wakubwa nchini wakitumika kama mabalozi kwa kuwawezesha kutembelea nchi husika na kutangaza fursa zilizopo huko basi bila shaka tutashuhudia ongezeko la vijana wengi kujihusisha na usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu nje ya nchi.

Mwisho kuna umuhimu wa serikali kuwahusha wadau kwenye sekta ya uvuvi kufanya tafiti za kisayansi juu ya mbegu bora za viumbe maji zitakazoweza kuleta ushindani kwenye masoko ya nchi husika, hivyo ni lazima njia za kisasa za kufuga viumbe maji zitumike ili kuleta uzalishaji wenye tija.