January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UVCCM yalaani kauli ya Gwajima

Na Joyce Kasiki,TimeMajira Online

JUMUIYA ya Umoja wa  Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa imelaani vikali kauli iliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa Kawe,  Askofu Josephat Gwajima ya kuhamasisha wananchi wasiende kupata chanjo huku wakisema ni utovu wa nidhamu kwa Rais Samia Suluhu na Serikali yake iliyoamus wananchi wachanjwe ili kuwakinga na corona.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa,Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Kenan Kihongosi amesema,Mbunge hiyo ambaye pia ni mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kitendo hicho alichokitafsiri kuwa ni dharau kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajia kuzindua kwa yeye mwenyewe kupatiwa chanjo.

“Juzi akihubiri kanisani kwake,Mbunge wa Kawe ndugu Gwajima alitoa mneno yasiyofaa kwa wananchi na maneno yale yamekuwa ni maneno ya kichochezi ,pia ni maneno ambayo yanaenda kuwagawa wananchi, kwani sababu mheshimiwa Rais na Serikali wameshatoa msimamo kwamba wananchi waweze kupata chanjo na chanjo imeshaletwa,” amesema Kihongosi na kuongeza kuwa,

 “Sasa anapojitokeza kiongozi mmoja katika mhimili anakwenda kuzungumza kanisani na kuwahubiria waumini ambao nao wana watu wengine nje kwamba anatuma sms kwamba chanjo haifai na ina madhara ,tunahoji yeye ni daktari alisomea? Amejuaje mambo haya hayafai,”

“Lakini  sambamba na hilo ni utovu wa nidhamu,maana serikali unataka kuwalinda wananchi na tumeona kwamba chanjo itakayotolewa kwa wananchi watakwenda kupata unafuu wa kujikinga na maradhi ya corona. Kwa hiyo sisi vijana wa Chama Cha Mapinduzi kauli zile tunazilaani na tunazipinga vikali,”amesema.