Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Mbozi.
MJUMBE wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM Taifa akiwakilisha Mkoa wa Songwe, Shaibath Kapingu,amewataka vijana wa chama hicho kutokubali kuwa machawa na wapambe wa watu,badala yake wahakikishe wanatunza taswira njema ya chama na viongozi walioko madarakani.
Amesisitiza kuwa kila mwanachama atakuwa na fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pindi uchaguzi utakapofika.
Kapingu amewataka vijana kuanza kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kuhakikisha wanagombea nafasi mbalimbali ili waweze kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Katika kikao hicho kilichofanyika Mlowo, wilayani Mbozi, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Songwe, Fatuma Hussein Mnahwate, aliwakosoa vijana wa vyama vya upinzani kwa kile alichodai kuwa wanashindwa kusema hadharani kwamba wanaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhofia viongozi wao wa juu.
Aidha, Mnahwate alieleza kusikitishwa na hali hiyo, akisisitiza kuwa vijana wa upinzani wanapaswa kuwa na msimamo wa kusema ukweli badala ya kuongozwa kwa hofu.
Kauli hizi zinakuja baada ya vijana wa CHADEMA na ACT Wazalendo mkoani Songwe kupinga madai kuwa wamekubaliana kumuunga mkono Rais Samia katika uchaguzi wa 2025, wakisema hakuna makubaliano yoyote kama inavyodaiwa na UVCCM.
Katika kikao hicho, viongozi wa UVCCM walipatiwa mafunzo kuhusu utendaji wa jumuiya hiyo na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla, huku Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Yusuph Ally Rajabu, akitoa elimu ya uenezi na uimarishaji wa chama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbozi, Majaliwa Mlawizi, kwa niaba ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) kutoka Songwe, Aden Mwakyonde, aliwataka viongozi wa UVCCM kuwa mstari wa mbele kulinda chama na kuwavuta vijana zaidi kujiunga na CCM.
MNEC huyo pia aliahidi kuchangia mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya katibu wa wilaya, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za vijana hao.



More Stories
Mahundi atembelea majeruhi wa ajali Mbeya
Jukwaa la usafiri Mtandaoni linavyotoa punguzo kwa abiria
Mbuja :Waliyoyapambania Wanawake wenzetu matunda yake tunayaona