November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UVCCM Ilemela kusheherekea miaka 59 ya Uhuru kwa kupanda miti

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

KATIKA kuadhimisha miaka 59 ya Uhuru wa Tanganyika, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Ilemela kwa kushirikiana na Chama hicho ngazi ya Wilaya kinatarajia kusherekea sikukuu hiyo kwa kupanda miti katika ofisi mpya ya Chama hicho ilipo Kata ya Buswelu.

Akizungumza na Mtandao huu kwa njia ya simu, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Ilemela Nehemiah Philimone amesema, kama UVCCM na Chama Wilaya ya Ilemela watashirikiana na Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Naibu Waziri Mteule wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula katika zoezi hilo la upandaji wa miti ikiwa ni sehemu ya kuweka kumbukumbu katika siku hiyo.

Nehemiah amesema, jumla ya miti 187 inatarajiwa kupandwa siku ya kesho ambayo imetolewa na Mbunge Dkt. Angeline Mabula ambaye ndiye mgeni rasmi katika zoezi hilo akiongozwa na Katibu wa CCM Wilaya hiyo Aziza Isimbula.

Amesema, lengo lao ni kuhakikisha wanatunza mazingira ili yaendane na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kuzuia mmomonyoko wa udongo ambao unaweza kujitokeza endapo kutakuwa na eneo ambalo halina miti.

Sanjari na hayo pia wanataka kuchochea na kuleta muungano baina ya chama na Serikali, kuleta ushirikiano wa pamoja kwa kuzingatia kauli mbiu ya ‘Tanzania yenye uchumi imara, itajengwa na Watanzania wenyewe, tufanye kazi kwa bidii, uwajibikaji na uadilifu’.

Pia amewasihi vijana kuweza kupanda miti katika maeneo yao na kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo pamoja na kujikita katika kufanya shughuli za kijamii, chama pamoja na kueleza yale yote yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa ustawi wa Taifa.