November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UVCCM Igunga wachangia damu chupa 58

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online,Igunga

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Igunga (UVCCM) umechangia damu chupa 58 kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto katika hospitali ya Wilaya hiyo zoezi ambalo limekwenda sambamba na hitimisho la ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

Miradi ya maendeleo iliyokaguliwa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Igunga, CDE Kimali Philipo Busakgala ni 14 ikiwa ni pamoja na zahanati ya kijiji cha Matinji ambao ujenzi wake umetekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani kiasi cha milioni ni 40,zahanati ya Ndembezi.

Pia shule ya msingi Ndembezi ambako kunajengwa matundu 26 ya vyoo vya walimu na wanafunzi ujenzi unaogharimu kiasi cha milioni 76 hadi kukamilika kwake.

“Shule ya sekondari Simbo kuna ujenzi wa matundu matano ya vyoo yanayogharimu kiasi cha milioni 9.8,ujenzi wa shule ya sekondari Mtunguru ambayo imepatiwa kiasi cha milioni 600.3, hapa tumegundua wizi wa vifaa unaofanywa na watumishi wa serikali pamoja na vibarua nimeisha toa maelekezo wahusika wote wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria,”amesema CDE Busagala.

Aidha miradi mingine aliyoitembelea na kuikagua ni ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Itunduru, ukarabati wa zahanati ya Mwandihimiji ambayo imepatiwa kiasi cha milioni 50.

Pia ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika sekondari ya Ibologelo yanayojengwa kwa fedha za ndani kiasi cha milioni 10.8, ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika sekondari ya Itumba iliyopatiwa milioni 10.8 kutoka Serikali Kuu.

Kadhalika ujenzi wa madarasa shule ya msingi Itumba iliyopatiwa milioni 40 kupitia mpango wa EP4R toka Serikali Kuu na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Bulyang’ombe.

“Tumeweza kufika na kukagua mradi wa vijana walio jiajiri kupitia mkopo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kiasi cha milioni 70 ambao wanajishughulisha na ufugaji wa kuku wa mayai na ufugaji wa samaki, kikundi hiki kinajulikana kwa jina la Poultray & Fish Farm,”.

Pia wamefika Igunga Mjini wamefika katika hospitali ya Wilaya kukagua na kupatiwa maelezo juu ya jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) litakalogharimu kiasi cha shilingi milioni 400 hadi kukamilika kwake.

Katika hatua nyingine, CDE Kimali Philipo Busagala ametembelea wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi namba 3 uliopo Kata ya Igurubi wa Mwekezaji Daud, mgodi namba 7 wa wachimbaji wadogo ambao wanatumia leseni ya Mzee Majour Bonny, mgodi namba 8 katika kijiji cha Matinje.

Aidha alitembelea mgodi wenye PML 0173 TBR unaomilikiwa na wawekezaji wadogo Pamela Joshua na Pendo Sundey nakutoa elimu ya usalama kwa wachimbaji ili kujikinga na majanga yanayoepukika katika maeneo yao ya uzalishaji dhahabu.

Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya ya Igunga Melchedes Magongo ameipongeza UVCCM kwa kuwatembelea na kujionea shughuli zinazofanywa na hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kukagua jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) na kuona umuhimu na thamani ya kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kuchangia chupa 58 za damu.

Kwa upande wake Pemela Jushua amewapongeza UVCCM Igunga kwa kuwatembelea na kukagua shughuli wanazozifanya wachimbaji wadogo ikiwa na kuendelea kuwakumbusha kufuata sheria ya usalama mahali pa kazi jambo ambalo limewafariji na kuona kuwa CCM ipo pamoja na wachimbaji na wananchi wake kwa ujumla.