November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uuzaji mafuta kwenye madumu, chupa wapigwa marufuku

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imewaagiza wamiliki wa vituo vya mafuta ya petroli nchini, kuchukua hatua stahiki,zinazozingatia usalama wa afya, mali na mazingira,katika uendeshaji wa biashara zao.

EWURA imetoa agizo hilo kutokana na kuongezeka kwa matukio ya milipuko ya moto,inayosababishwa na uuzaji holela wa mafuta ya petroli kwa kutumia madumu au chupa.Jambo hilo ni kinyume na tahadhari za usalama wa afya, mali na mazingira (HSE).

Taarifa iliyotolewa Septemba 16, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, imewasisitiza wafanyabiashara wa vituo vya mafuta nchini, kutoruhusu uuzwaji wa mafuta katika vifaa visivyoruhusiwa, kwa ajili ya kubebea mafuta ya petroli kama vile madumu, chupa aina zote na vifaa vingine.

“Tunawahimiza wamiliki wa vituo vya mafuta, kuchukua tahadhari kwa kuzingatia matakwa ya kanuni ya 27, inayosimamia biashara ya vituo vya mafuta nchini,”.

Hata hivyo, EWURA imebainisha kuwa, itaendelea kufanya ukaguzi kwenye vituo vya mafuta nchini nzima, ili kuhakikisha utekelezwaji wa kanuni hizo.Huku ikitoka onyo kwa yeyote atakayekiuka kanuni hizo,hatua kali za kisheria ziatachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufungiwa vituo vyao.