January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uturuki yampuuza Rais Joe Biden

ANKARA,Serikali ya Uturuki ambaye ni mshirika wa Marekani na mwanachana wa Jumuiya ya kujihami NATO, imepuuzilia mbali tamko la Rais Joe Biden la kuyatambua mauaji ya Waarmenia kuwa ya Kimbari.

Uturuki imesema hatua hiyo ni ya kutafuta na kujipa fursa kisiasa na ni usaliti mkubwa kwa amani na haki.

Kutokana na hatua hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesema itamuita balozi wa Marekani nchini humo ili kuelezea kujitenga kwake na kauli ya Biden.

Msemaji wa rais wa Uturuki, Ibrahim Kalin amesema Biden anapaswa kuangalia kwanza historia ya Marekani kabla ya kuanza kuwakosoa wengine.

Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kutumia neno mauaji ya kimbari kuyaelezea mauaji ya Waarmenia ya mwaka 1915 yaliofanywa na askari wa utawala wa Ottoman.

Tamko hilo lilitolewa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji hayo. Rais Biden amesema hatoi lawama kwa mtu yeyote, lakini anajaribu kuhakikisha kilichotokea hakitajirudia tena katika Dunia ya sasa.