Judith Ferdinand
Kukua kwa teknolojia duniani kumesaidia wasichana na wanawake kupata vifaa bora vya kujihifadhia wakati wa hedhi ikiwemo taulo za kike(peds) hivyo kuwafanya kujiamini na kuwa huru wakati wote.
Licha ya vifaa hivyo kuwa msaada imeelezwa kuwa kumekuwa na changamoto kwa jamii(wanawake na wasichana), kushindwa kuhufadhi vyema taulo za kike zilizotumika na badala yake wamekuwa wakitupa ovyo mitaani na kusababisha uchafuzi wa mazingira pamoja na kuhatarisha afya kwa wakazi wa eneo husika.
Baadhi ya wananchi mkoani Mwanza wanenaWakizungumza na Timesmajira online baadhi ya wakazi wa mkoani hapa wameeleza kuwa tabia hiyo ya baadhi ya wanawake na wasichana kutupa taulo za kike baada ya kutumia imekuwa kero licha ya kuchafua mazingira pia ni kitu cha aibu.
Agnes Lucas mmoja wa wananchi wa mtaa wa Mkudi wilayani Ilemela mkoani Mwanza, ameeleza kuwa kumeibuka tabia mbaya ndani ya jamii ambapo unakuta taulo za kike zilizotumika zikiwa zimezagaa ovyo mitaani kitu ambacho ni hatari kwa afya hususani watoto wadogo ambao hawaelewi chochote wanaweza kuokota na kuchezea na wakati huo uwezi jua aliyetumia kifaa hicho alikuwa na magonjwa gani.
“Kadri siku zinavyoenda ndivyo utupaji wa taka hizo umeshika kasi hii inaonesha ni kwa namna gani wamama tumesahau mila na desturi zetu na kushindwa kuwafundisha mabinti zetu namna ya kuhifadhi taulo za kike baada ya kutumia pamoja na hatari ya kuzitupa ovyo,”anaeleza Agnes na kuongeza kuwa
“Mtu anapoingia katika hedhi ni jambo la siri ambalo mtu mwingine hapaswi kuona uchafu wake lakini sasa ukipita kwenye mitaa hususani kwenye maeneo ambayo makazi yake yamebanana unakuta taulo za kike zilizotumika zikiwa zimezagaa ovyo ambapo mbali na kuchafua mazingira pia ni aibu tunawaonesha nini wanaume pia tunawafundisha nini watoto wetu wa kike maana hali hii ikiendelea baadae wakikua wataona ni kawaida,”.
Naye Idd Mumba mmoja wa wakazi wa jijini Mwanza, anaeleza kuwa suala la vifaa vinavyotumika kuwastili wasichana na wanawake wakati wa hedhi imekuwa changamoto katika kutunza baada ya kutumia.
“Kwenye matumizi wanatumia vizuri ila kuzihifadhi baada ya matumizi imekuwa changamoto kwa sababu kuna baadhi yao siyo wote wanatupa ovyo eneo lolote na hawazihifadhi vile inavyotakiwa kwa sababu zile ni taka pia kwani kwa kuheshimu siku za hedhi mwanaume anashindwa kukutania naye kimwili lakini unapokuta zimetupwa ovyo baada ya kutumika najihisi ukinyaa kabisa nikiona zikiwa zimezagaa,”.
Mumba ameishauri kuwa zile taasisi na kampuni zinazozalishwa na kusambaza taulo hizo za kike shuleni au sehemu yoyote wangekuwa toa elimu kama wanavyotoa ya namna ya kutumia basi na wakimaliza kutumia wafanyeje ili kuzihifadhi na kuacha uchafuzi wa mazingira ambao yeye binafsi anaona kinyaa.
“Tutunze mazingira na wasichana waendelee kujistiri wakiwa katika siku zao huku viongozi kwa ujumla kuanzia Kijiji hadi Mkoa kwenye vikao na mikutano ya hadhara watoe elimu ya juu ya namna ya kutunza taulo za kike baada ya kuzitumia,hiyo itasaidia kutunza mazingira na ukiangalia pedi zikirundikana sana itasababisha eneo husika ata majani yasiote hivyo kuwa na uchafunzi mkubwa wa mazingira,”anaeleza Mumba.
Anaeleza kuwa pia baadhi ya wanafunzi wa kike mazingira ambayo wanatupia taka hizo baada ya kujistiri siyo rafiki na uchafuzi wake unakuwa mkubwa na katika kipindi hiki cha kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanatakiwa waanze na vitu kama hivyo vidogo ambazo wakiviachia vitaleta athari kubwa.
“Kwaio tuanze sasa hivi kuwaelimisha kuwa ikitokea mtu ametumia taulo za kike akimaliza matumizi yake ajue atakihifadhi wapi kama ni kuchoma ahakikishe kimeungua chote na kama ni kuchimba shimo afukie afanye hivyo ili kulinda mazingira na mtu asikute ikiwa imezagaa tu hii ikiwa ni sambamba na mipira ya kiume ambayo haiozi hivyo inachafua mazingira unakuta watu wa nyumba za kulala wageni wanakuwa wanazitupa ovyo kikubwa elimu itolewe ili tuweze kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,”.
Ofisa Maendeleo ya Watoto shirika la Mtandao wa Vijana na Watoto Mwanza (MYCN)Nuru Massanja,anaeleza kuwa kulingana na tamaduni mbalimbali zipo jamii ambazo haziamini katika kutupa taulo za kike zilizotumika badala yake wanaamini katika kufikia na kuchoma ila kuna wengine hawajali bali wanatupa ovyo.
Hivyo kutokana na jambo hilo elimu inahitajika kutolewa kwa jamii juu ya namna gani nzuri ya kutunza taulo za kike zilizotumika ili kuacha kuchafua mazingira yanayochochea mabadiliko ya tabianchi.
“Ingawa ni changamoto kumueleza mtu atupe taulo yake ya kike iliotumika katika chombo cha taka mfano kilichopo stendi ataona ametenda kinyume na tamaduni yake hivyo anaona abebe akatupie nyumbani kwaio elimu inahitajika kuhusiana na kuacha tamaduni ya kizamani,tutupe pedi zetu katika mazingira ambayo ni rafiki ambapo siyo barabarani,katika mitaa viongozi wa kata na mitaa watoe elimu pia juu ya namna bora ya kuhifadhi pamoja na kuwezesha vifaa vya kutunzia uchafu huo katika mitaa,”.
Kwa upande wake Anitha Samson kutoka shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence, anaeleza kuwa licha ya kuwa shirika lao linasaidia wasichana taulo za kike lakini limekuwa likiwapa elimu juu ya namna ya kutunza baada ya kutumia kwani utupaji wake ovyo unakuwa unadharirisha utu pamoja na kusababisha suala la uchafuzi wa mazingira kwenye jamii.
“Tumekuwa tunawaelekeza namna ya kuzitunza au kuzitupa ikiwa ni pamoja na kuzichoma au kuzitupa kwenye vyoo vya shimo siyo tofauti na hapo maana yake kuzifukia chini zitaweza weA kuibuka juu na kuleta taharuki kwenye jamii hivyo tumekuwa tukiwafundisha namna ya kutumia pedi pia na usafi wa mazingira na maeneo wanayoishi kwani tunaposema hedhi salama ni pamoja na maeneo wanayoishi kwani kutupa pedi ovyo ni kuhatarisha afya ya jamii na yake binafsi,”anaeleza Anitha.
Pia anaeleza kuwa suala la hedhi salama ni pamoja na kutunza taulo za kike zilizotumika vizuri ikiwa ni pamoja na kuzichoma moto au kutupa kwetu choo cha shimo na wasiweke kwenye vyoo vingine vinaziba.
Anaeleza kuwa wamekuwa wakihamasisha maeneo ya shule kuhakikisha kunakuwa na vichoma taka ambavyo vitatumika pia kuchomea taulo hizo zilizo tumika ingawa changamoto iliopo ni baadhi ya wanafunzi kulalamika kuwa zinakaa muda mrefu kwenye vyombo vya kutunzia taka kabla ya kuchomwa hali inayosababisha wakati wakienda kuzichoma moto zinatoa harufu huku zikiwa na wadudu.
“Tunashauri shule kufanya utaratibu wa kila mwanafunzi kutupa taulo yake ya kike iliotumika kwenye kifaa cha kichomea moto mwenyewe kwani kuchoma za mtu mwingine kiafya siyo nzuri na inaleta hali mbaya kwa wanafunzi wanaochoma taulo hizo pia kwa sehemu yenye watoto wengi kuwe na choo cha shimo kwa ajili ya kutupia taka hizo,”.
Mwandishi wa Habari wa Azam Tv Mkoa wa Mwanza Innocent Aloyce,anaeleza kuwa kuhusiana na utupaji wa wa baadhi ya vitu ambavyo vimekuwa vikitumika katika maeneo ya usiri hasa taulo za kike wanzotumia wasichana na wanawake, pampers kwa watoto na mipira ya kiume (kondomu) imekuwa changamoto hasa kwenye maeneo ambayo wanaishi watu wa maisha ya chini au mifumo ya maisha ni ya kawaida sana.
“Maisha yao yanakuwa siyo rafiki ya kipato ata mazingira tukienda kwenye maeneo ya visiwani na mialo tumeshuhudia sana hivyo vitu vikiwa vinatupwa bila kufuata utaratibu,”.
Innocent anaeleza kuwa hivyo hali hiyo imekuwa changamoto kwanza kwa mtu kuona vitu hivyo hadharani haileti picha nzuri kwa sababu vimekuwa vikitumika kwenye sehemu za usiri wa viungo vya binadamu.
“Mfano mtu anatupa taulo za kike ambazo tayari zimeisha tumika ile inakuwa na uchafu wa damu hatujui huyo mtu alikuwa anaumwa ugonjwa gani au alikuwa anafanya nini lakini pia kuna wanyama kama paka na mbwa wanaweza kuchukua taulo hizo wakapita nazo sehemu mbalimbali kwani baadhi ya wanyama uchafu ndio sehemu ya maisha yao hivyo kidogo imekuwa changamoto ya kusambaza magonjwa kwa baadhi ya maeneo,”anaeleza Innocent na kuongeza kuwa
Anaeleza kuwa kitu anachoona ndio sababu kubwa ni watu kutokuwa na uelewa hasa ya namna gani watahifadhi hivyo vitu baada ya kutumia na hiyo ndio imekuwa changamoto.
Hivyo wadau na wazalishaji wa bidhaa hizo za kujihifadhia waone namna bora ya kuwaelimisha wateja wao namna bora ya kuhifadhi au kuteketeza vitu hivyo baada ya kutumika.
“Nashauri kwanza watengenezaji wa bidhaa hizo kama tunavyoona kwa sasa kwenye kampuni zinazotengeneza maji kwenye chupa za maji kuna alama inaonesha namna mtu anavyoweza kutupa chupa ya maji sehemu husika baada ya kutumia bidhaa hiyo hivyo utaratibu huo ufanyike pia kwa wazalishaji wa bidhaa hizo kwa kuwaelimisha wananchi ikiwa ni pamoja na kutengeneza maelezo ya kuhifadhi na kuteketeza vitu hivyo baada ya kutumia,”.
Pia anaeleza kuwa elimu itolewe kwa jamii kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa au wa mama watu wazima katika jamii waelekezane pale wanapoona watoto wao wa kike wamekuwa kwa kuwaeleza ni namna gani taulo za kike baada ya kutumia zinapaswa kuhifadhiwaje.
Aidha kwa vijana wa kiume wawaeleze kuwa baada ya kutumia mipira ya kiume inatakiwa kuhifadhiwaje kadhalika katika pampers kuwa na namna bora ya kuvitunza na kuvihifadhi hivyo vitu pale vinapokuwa vimeisha tumika.
Akizungumzia nafasi ya mwandishi wa habari katika suala hilo Innocent anaeleza kuwa waandishi wa habari Wana nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii.
“Usishangae pia kuona waandishi wa habari baadhi nao wakawa ni sehemu ya kuchafua mazingira kwaio suala hili lianzie ngazi ya familia ni kweli sisi wanahabari ni wajibu wetu lakini pale ambapo tutajengewa uelewa juu ya changamoto hii na kwa pamoja tutaona kwa namna gani tutakuwa na kampeni ya kuelimisha jamii kupitia kalamu zetu juu ya suala hili,”.
“Pia itasaidia kuona jamii katika maeneo yetu inaanza kubadilika kwanza kwa kupunguza athari za kimazingira kutokana na hivyo vitu pili kutunza heshima kwenye jamii kwa maana lwa sasa kwenye jamii kumekuwa na mmomonyoko wa maadili ambao unaanzia”
“Huku kwa mtoto kuona taulo za kike zilizotumi, pampers au kitu kingine cha sirini hivyo ataona ni kitu cha kawaida,tunatengeneza kizazi ambacho hakishangai vitu vya sirini hadharani wakati sisi tunakuwa kuona nguo ya ndani imeanikwa nje ilikuwa kitu cha ajabu sana ila siku hizi ni kawaida hivyo ipo haja ya kushirikiana waandishi na wadau ilikuwa kuwa na jamii salama zaidi,”.
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) Kanda ya Ziwa Victoria NEMC Jarome Kayombo,anaeleza kuwa kumekuwa na changamoto ya utupaji wa taulo za kike zilizotumika, ambapo wakirudi kwenye sheria ya mazingira imefafanua wajibu,haki wa idara,Wizara,Mamlaka na Mwananchi mmoja mmoja.
“Ukija katika suala zima la usimamizi wa taka ngumu kwa mujibu wa sheria inasimamiwa na halmashauri moja kwa moja lakini sisi Nemc siyo kama tumekaa kimya tunaendelea kuunga mkono kwa kutoa elimu na ushauri wa kitaalamu na tunapoona Halmashauri imezidiwa tunaingia moja kwa moja kusimamia,”anaeleza Kayombo.
Akizungumzia utupaji wa taulo za kike zilizotumika mfano kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ikiwemo shule za bweni,vyuo Kayombo anaeleza kuwa zamani mama zetu walikuwa na namna yao wanaweza kujihifadhia lakini kwa sasa teknolojia imekua hivyo zimekuja taulo za kike lakini utunzaji wake baada ya matumizi siyo mzuri.
“Ebu fikiria mfano kama chuo kina wanafunzi wa kike 3000 maana yake kila mwezi kama mtu anaingia hedhini siku nne hadi tano na kwa siku labda anabadili moja moja maana yake kwa mwezi mtu mmoja utazalisha taka hizo za taulo za kike zilizotumika zaidi 4 kuwa na zaidi ya taulo hizo zilizo tumika 8000, kutoka kwenye eneo moja mfano shule au chuo na kwa Mwanza tuna vyuo vingi na ni kweli tukipita maeneo ya vyuo ukiangalia katika eneo la taka zinapokusanywa utakuta asilimia kubwa ni hizi taulo za kike zilizotumika,”anaeleza Kayombo.
Lakini pia anaeleza juu ya matumizi ya pampers kwa watoto,ebu fikiria kwenye mtaa wenye watoto 50, labda kwa siku mtoto mmoja anabadilisha pampers tatu hivyo kwa siku unakuta mtaa unazalisha taka ngumu zinazotokana na pampers 150.
Kimsingi taulo za kike na pampers ni teknolojia nzuri ya kuwastili wanawake,wasichana na watoto lakini kama nchi wanatakiwa wajue wanazihifadhi vipi baada ya matumizi ili zisisababishe uchafuzi wa mazingira.
“Ni kweli kwamba tunapozungumzia taulo za kike zikiisha tumika zina hama kutoka kwenye taka na kuwa taka hatarishi mwisho wa siku zinakuwa na athari zaidi ikiwemo magonjwa vile vile kwa pampers,”anaeleza Kayombo.
Nini kifanyike katika kudhibiti utupaji wa taulo za kike zilizotumika ovyoKayombo anaeleza kuwa suala la kudhibiti utupaji wa taka hizo wasiiachie Halmashauri pekee yake kwani siyo Halmashauri zote zinavitendea kazi na miundombinu ya kusimamia na kudhibiti taulo za kike na pampers zilizotumika kiasi kwamba zimekuwa zigizaagaa kwenye jamii.
“Enzi tupo wadogo tulikuwa hatujui kama mama na dada zetu kama walikuwa na hali ya hedhi kwa sababu walikuwa wanajua namna ya kujistiri lakini Sasa hivi ukipita mitaani unakuta taulo ya kike imetumika imetupwa nje pampers inakinyesi imefungwa fungwa na kutupwa nje alafu kesho kikitoka kipindupindu tunalalamika”anaeleza Kayombo.
Anaeleza kuwa hoja hiyo kuitatua inawapasa kukaa pamoja kulijadili na kilitafutia muafaka huku Nemc wanafanya na kwa sasa wanaishukuru Wizara ya Elimu inasajili miradi kwa ajili ya kufanya tathimini ya athari za mazingira na moja ya kigezo ambayo watapitisha katika miradi hii ni shule kuwa na kichomea taka hususani zinazobeba watoto zaidi ya 1000.
Anafafanua kuwa kila shule na vyuo vyote viwe na vichomea taka ili hawa wasichana baada ya kujihifadhi na kuzikusanya taulo za kike zilizotumika basi zikachomwe ili kutochafua mazingira na wameisha anza kwa baadhi ya chuo na shule kuwa moja ya masharti ni kuwa na kichomea taka.
“Unajenga chuo na unategemea kitakuwa na bweni na watoto wa kike watakuwepo hakikisha kunakuwa na kichomea taka lakini pia tunahamasisha halmashauri upande wa hospitali zimekuwa na vichomea taka lakini sasa ni wakati wa kuhakikisha hata madampo yetu yawe na vichomea taka ili tukiisha kusanya taka kutoka kwenye mitaa mbalimbali tutenge taka hatarishi kama taulo za kike na pampers ziwe na gari lake na zikifikishwa dampo zikachomwe,”anaeleza na kuongeza kuwa
Pia anato wito kwa watumiaji wa taulo za kike na pampers pamoja na wananchi kwa ujumla mmoja mmoja wanatakiwa kubadilika tabia kwa kuanza kuzitenga taka yani mabaki ya chakula yakae sehemu yake na taka hatarishi taulo za kike na pampers zikae sehemu yake ili ata yule atakayekuja kuchukua taka tumkinge.
“Tukiangalia hili kwa ukaribu na kutembea nayo pia ukikaa na watu wa Mwauwasa ukawauliza kwanini mifumo yao ya majitaka inaziba mara kwa mara watakuanbia watu wanatupa aidha taulo za kike au pampers zilizotumika katika miundombinu yao,matokea mifumo inaziba serikali kuingia gharama kubwa hivyo kila Mtanzania kufikiria namna bora ya kuhifadhi taka hizo kwa kuwekeza katika miundombinu na kutenga taka nyumbani mwetu tunapozizalisha”.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Dkt.Sebastian Pima,anaeleza kuwa suala la utupaji wa taulo za kike ovyo ni hatari kwa afya.
“Taulo za kike zilizotumika ni uchafu kama uchafu mwingine lakini pia zinakuwa na damu ambayo inaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa mfano mtu ambaye katupa taulo hiyo ya kike alikuwa na maambukizi ya VVU hivyo mtoto akachukua na kuanza kuchezea anaweza kupata maambukizi pia hivyo ikawa ni chanzo cha maambukizi ya magonjwa,”anaeleza Dkt.Pima.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia