March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utunzaji wa mazingira wazalisha biashara ya kaboni Katavi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoka amesema Utunzaji wa Mazingira, Misitu na vyanzo vya Maji, umewezesha Mkoa kuingia kwenye biashara ya Kaboni (hewa Ukaa) katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambapo hadi kufikia Juni, 2025 Mkoa umefanikiwa kupata mapato jumla ya Shilingi 25,293,421,607.17.

Ambapo imefanikisha ujenzi wa  Madarasa 52, Kukarabati Madarasa 20, ujenzi wa nyumba 5 (2 kwa 1), ujenzi  wa nyumba 1 (3 kwa 1), ujenzi wa vichomea taka 6 (Incenerators), ujenzi wa mashimo 6 ya kondo la Mama (Placenta pits) kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, ukamilishaji wa Zahanati 1, ujenzi wa matundu 128 ya vyoo, utengenezaji wa madawati 1,496, ujenzi wa Ofisi za vijiji 8, ujenzi wa Masoko 2 ya vijiji 2, ajira  112 kwa Vijana wanaolinda Misitu, utoaji wa kadi za Bima ya Jamii – CHF iliyoboreshwa (iCHF) za Afya kwa kaya 4,400, Ajira za walimu 20 wa mikataba, Utoaji wa chakula cha wanafunzi kwenye Shule 16 na utoaji wa mikopo yenye thamani ya shilingi 117,213,800.00 kwa Wanawake wajasiriamali.

RC Mrindoko amesema hayo jijini hapa leo,Julai 3,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema  kupitia fedha hizo bilioni 2,782,421,607.17 za biashara ya kaboni zilizopokelewa Mwezi Aprili.

“2025 Mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika umepanga kuendelea Kujenga na kukarabati miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari, Kuboresha na kuimarisha uhifadhi na utunzaji wa rasilimali Misitu, Kutoa ajira za mkataba kwa watoa huduma wa Afya katika Zahanati za Vijiji na Walimu,”amesema.

Vilevile Mrindoko amesema kuwa Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi za uwekezaji hapa nchini ikiwemo uzalisha chakula ambapo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 ya watu na makazi, mkoa wa Katavi una idadi ya watu 1,152,958 ikiwa ni ongezeko la watu kwa asilimia 7.2 na ndio mkoa unaoongoza kwa kuongezeka kwa wingi zaidi idadi ya watu hapa nchini kulinganisha na mikoa mingine.

“Sababu ya ongezeko hili ni fursa nyingi zilizopo mkoa huu ambazo ni Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Madini, Viwanda, Biashara ikiwemo ya mazao, madini ya dhahabu, shaba, Utalii, Maliasili na nyinginezo nyingi ambazo zimekuwa ni kimbilio la wananchi wengi mkoani humo hasa wanaotoka Miko ya Ukanda wa Ziwa Victoria.

“Mkoa wetu unakua na mkoa huu una fursa nyingi za uwekezaji, kwenye sekta ya kilimo, sekta ya mifugo, sekta ya madini, viwanda, biashara ya mazao, biashara ya madini na kadhalika. Na kwa maana hiyo, Mkoa wa Katavi ni kweli kabisa umekuwa kimbilio la watanzania wanaohama kutoka mikoa mbalimbali na hasa mikoa ya ukanda wa Ziwa Victoria wanahamia kwa wingi,”amesema.

Pamoja na hayo amezungumzia ujenzi wa barabara ambapo amesem kuwa kuna  barabara ya Kagwira- Karema inayojengwa mkoani Katavi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) yenye urefu wa Kilomita 110.29 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Shilingi Bilioni 112.141 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao 2026.

“Kukamilika kwa barabara hii kutaufungua Mkoa wa Katavi kibiashara na nchi za Congo na Burundi kupitia Bandari ya Karema iliyopo Wilaya ya Tanganyika mkoani humo ambako barabara hiyo inaishia hasa biashara ya mazao ya kilimo na mifugo,”amesema.